Azam yajipanga kufanya makubwa michuano CAF

24Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Azam yajipanga kufanya makubwa michuano CAF

BAADA ya kukamilisha usajili wa wachezaji wanne wapya, mabosi wa Azam FC wamesema lengo la kuboresha kikosi chao ni mahitaji ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya kimataifa.

Azam FC ambayo imemaliza msimu uliopita katika nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa Simba na Yanga iliyoshika nafasi ya pili, ni moja kati ya timu nne za Tanzania zitakazoshiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, alisema wanataka kuona msimu ujao wanafanya vyema na kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Simba katika michuano ya kimataifa msimu uliomalizika.

Alisema Simba walipambana hadi kufikia hatua ya robo fainali, hivyo msimu ujao wanatakiwa kuunganisha nguvu kufika mbali zaidi na hivyo Tanzania kupata heshima.

Alisema bado hawajamaliza mchakato huo wa kukijenga kikosi chao kwa sababu wanafahamu ushindani kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa msimu ujao itaongezeka kutokana na kila timu haitaki kuwa wasindikizaji.

Nyota wapya ambao tayari Azam FC imeshawasajili ni pamoja na mshambuliaji wa Gor Mahia ya  Kenya, Kenneth Muguna,  kiungo mshambuliaji Mzambia, Charles Zulu  akitokea Cape Town City ya Afrika Kusini na straika wa Timu ya Taifa ya Zambia, Rodgers Kola ambaye amemaliza mkataba wa kuitumikia Zanaco.

Kwa upande wa hapa nchini, matajiri hao wa Chamazi wamekamilisha usajili wa beki wa kushoto, Edward Charles Manyama kutoka Ruvu Shooting ya Mlandizi mkoani Pwani.