Azam yajipanga kumlinda Dube

18Oct 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Azam yajipanga kumlinda Dube

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC, wamesema hawana mpango wala mawazo ya kumuuza mshambuliaji wao anayefanya vyema, Prince Dube, imeelezwa.

Dube ambaye anaongoza katika kupachika mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, akifunga magoli sita, ameanza kuwindwa na timu mbalimbali baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye mechi zote sita alizocheza.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulrahman Amin 'Popat' aliliambia gazeti hili jana ni mapema sana kuzungumzia suala la kumuuza mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe ambaye ameitumikia klabu hiyo kwa muda mfupi.

"Hatujapokea ofa yoyote, yanayoendelea katika mitandao ni uongo, Dube amesaini mkataba wa miaka miwili na ndio kwanza ameitumikia klabu kwa miezi miwili tu, lengo letu msimu huu ni kutwaa ubingwa," alisema Popat.

Aliongeza usajili walioufanya msimu huu ulilenga kuipa mafanikio klabu yao na wanashukuru kupata matokeo mazuri kwenye mechi zote sita walizocheza za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Gazeti moja la Zimbabwe limeandika klabu ya Raja Casablanca ya Morocco imeonyesha nia ya kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo ambaye Septemba alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi.

Kikosi cha Azam FC kinaendelea na mazoezi kwa ajili ya mchezo wao unaofuata dhidi ya Ihefu FC utakaofanyika Oktoba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mwanza.

Habari Kubwa