Azam yapanga kuwakabili Pyramids mapema mchana

14Oct 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Azam yapanga kuwakabili Pyramids mapema mchana

KLABU ya Azam FC imesema mechi yao ya raundi ya kwanza ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids kutoka Misri itachezwa kuanzia saa 9:00 mchana keshokutwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zacharia, alisema mpaka sasa bado hawajapata taarifa yoyote kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kama watapata ruhusa ya kuingiza mashabiki, lakini juhudi bado zinafanywa ili kuomba ruhusa.

Zakaria alisema uamuzi wa kucheza mchana umefanywa kwa mapendekezo kutoka kwa benchi la ufundi na si kulenga kuwachosha wapinzani wao.

"Sijafanya utafiti wa kutosha kuwa Waarabu wanapata tabu wakicheza kwenye mazingira ya jua kali, lakini mimi ninavyojua tupo ndani ya kanuni wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inayosema unaruhusiwa kucheza mechi za kimataifa muda wowote kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa nne usiku, kwa hiyo sisi tumeamua kucheza muda huo," alisema Zacharia.

Aliongeza timu yao inaendelea vyema na maandalizi na wanaamini wachezaji watapambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.

"Tena kama maombi yetu yatakubaliwa ya kuingiza kiasi cha mashabiki kama tulivyoomba CAF kupitia TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), itakuwa vizuri zaidi kwa sababu mechi ikianza muda huo itaisha mapema na mashabiki watarudi makwao mapema sana," Zacharia alisema.

Alisema pia kikosi chao kimeendelea kuimarika na mchezaji ambaye ni majeruhi ni Prince Dube, huku akiwatoa hufu mashabiki wa Azam waliokuwa na wasiwasi juu ya wachezaji wao waliokwenda kuzitumikia klabu zao za taifa kwenye michuano ya kusaka tiketi ya kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar Ukanda wa Afrika, kuwa wote wamesharejea.

"Tunashukuru kikosi kimekamilika, wachezaji waliokwenda kutumikia mataifa yao wote wamesharejea na wanaendelea na programu za klabu, akili yetu ni kuona tunapambana ili kupata matokeo mazuri hapa nyumbani na baadaye kwenda Misri kukamilisha kazi," aliongeza kiongozi huyo.

Pyramids ilitarajiwa kuwasili nchini jana saa 3:00 usiku tayari kwa mechi hiyo, huku mchezo wao wa marudiano ukitarajia kuchezwa Oktoba 23, mwaka huu nchini Misri.

Timu nyingine za Tanzania zilizobakia katika mashindano ya kimataifa ni Biashara United ya Musoma inayopambana kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wao wanapeperusha bendera ya nchi katika kinyang'anyiro cha Ligi ya Mabingwa Afrika.

Habari Kubwa