Azam yataja sababu ya kuwaacha wa kimataifa

26Jul 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Azam yataja sababu ya kuwaacha wa kimataifa

UONGOZI wa Azam FC, umetoa sababu ya kuachana na nyota wake wanne wa kimataifa kutokana na kushindwa kupata namba ndani ya kikosi cha kwanza kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam imeachana na beki wa kati, Yakubu Mohammed, kiungo Ally Niyonzima, mshambuliaji, Mpiana Monzinzi walioingia makubaliano ya kuvunjiwa mkataba na Obrey Chirwa ambaye mkataba wake umemalizika.

Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria, alisema uamuzi wa kuachana na nyota hao ni baada ya mapendekezo ya Kocha Mkuu, George Lwandamina kutokuwa katika mipango yake kwa msimu ujao.

Alisema wanawashukuru kwa mchango wa nyota wao walioutoa katika timu hiyo kwa kipindi chote kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi na kushindwa kupata nafasi ndani ya timu wameamua kuachana nao.

"Hivi karibuni wamekosa nafasi ya kucheza ndani ya kikosi cha kwanza, kulingana na wao wachezaji wa kigeni tumeona busara kuachana nao ili kwenda kutafuta timu nje ya Azam FC ili kulinda vipaji vyao.”

"Kuondoka kwao hao kunatoa nafasi ya waliosajiliwa kulingana na mapendekezo ya kocha Lwandamina kuchukuwa nafasi zao, kwa lengo la kuimarisha kikosi chetu kuelekea msimu ujao," alisema Zakaria.

Alisema wachezaji waliosajiliwa ni mapendekezo ya kocha huyo ambaye wengi wao aliwakilisha majina ya nyota hao na wengine nafasi kulingana na mahitaji yao kwa msimu ujao.

"Msimu ujao tuna nafasi ya kucheza kombe la Shirikisho Barani Afrika (FA), tunapaswa kusajili wachezaji ambao watasaidia timu kwa ajili ya kufikia malengo katika michuano hiyo pamoja na kufanya vizuro katika ligi yetu ya nyumbani," alisema Zakaria.

Uongozi wa Azam FC tayari umewatambulisha nyota watano, wanne wa kimataifa ambao ni Mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Rodgers Kola (Zanaco), kiungo mshambuliaji wa Zambia na Cape Town City ya Afrika ya Kusini, Charles Zulu.

wengine ni kiungo mshambuliaji wa Kenya, Kenneth Muguna (Gor Mahia), kiungo mkabaji wa Zambia, Paul Katema, (Red Arrows) na beki iwa kushoto wa kimataifa wa Tanzania, Edward Manyama kwa usajili huru akitokea Ruvu Shooting.