Azam yatuma shushushu Shelisheli

18Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Azam yatuma shushushu Shelisheli

KATIKA kuhakikisha inafanya vizuri katika michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Azam FC ilituma shushushu Shelisheli mwishoni mwa wiki kuzisoma kiufundi timu za Bidvest Wits ya Afrika Kusini na Light Stars, ambazo mojawapo watakutana nayo katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho.

AZAMU

Makocha wasaidizi wa Azam, Mario Marinica na Dennis Kitambi, walikuwapo Shelisheli Jumamosi kushuhudia mchezo wa raundi ya awali ya michuano hiyo, Bidvest Wits ikishinda 3-0.

Kitambi alikaririwa kwenye mtandao rasmi wa Azam FC jana akieleza kuwa Bidvest ilitumia zaidi kikosi cha wachezaji wengi vijana na kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wake wa kikosi cha kwanza.

“Dhumuni letu kwenda kule tulikuwa tunataka kuwaona wapinzani wetu tutakaocheza nao katika raundi inayofuata, tunajua ya kuwa tutakutana na Bidvest katika raundi ijayo kutokana na aina ya mpinzani waliokutana naye, lakini tulikwenda kule (Shelisheli) kuhakikisha tuwaona Light Stars namna wanavyocheza, huwezi kujua lolote linaweza kutokea kwenye soka.

“Bidvest tulishawasoma kwenye mechi zao nyingi za Ligi Kuu Afrika Kusini na tunazo baadhi ya DVD zao, lakini tulichokiona kule ni wao kutumia kikosi cha vijana zaidi na ni tofauti na mechi zao za ligi,” alisema Kitambi.

Kocha huyo wa zamani wa Ndanda FC alisema watakuwapo pia Afrika Kusini kuwasoma tena Bidvest Wits katika moja ya mechi yao ligi ili kuijua kiundani zaidi timu hiyo ya kocha Gavin Hunt.

Azam FC imejiwekea lengo la kutinga hatua ya robo-fainali msimu huu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo, Azam FC ndio timu pekee ya Afrika Mashariki iliyoanzia raundi ya kwanza. Timu hiyo ya Chamazi itaanzia ugenini kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kurudiana Dar es Salaam kati ya Machi 18, 19 na 20.