Azam yazipotezea Simba, Yanga mbio ubingwa

20Apr 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Azam yazipotezea Simba, Yanga mbio ubingwa

KOCHA Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, amesema hawana muda wa kuwatazama Simba na Yanga wanafanya nini zaidi ya wao kuhakikisha wanaonyesha kiwango bora na kutafuta matokeo kwa kila mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na gazeti hili jana, Vivier alisema malengo makubwa ni kupambana kutafuta nafasi mbili za juu, ubingwa au nafasi ya pili ambazo zitawafikisha katika malengo yao ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa msimu ujao.

Alisema wanapamba kuhakikisha wanashinda mechi zao bila kuangalia wanaowafuata na waliopo juu yao wanafanya nini, zaidi ya kupigania kumaliza michezo yao kwa kupata ushindi.

"Tunahitaji kushinda mechi zetu zote, bila ya kuangalia waliokuwa juu, kuhakikisha kila mechi kwetu tunahitaji kupata matokeo mazuri ili kufikia malengo yetu ya kumaliza tukiwa katika nafasi mbili za juu," alisema Vivier.

Alisema wanaendelea vizuri na maandalizi yao huku wakifanyia kazi upungufu unaojitokeza katika kila mechi ikiwamo safu ya ulinzi kutoruhusu mabao na washambuliaji kutumia vema nafasi wanazozitengeneza kupata mabao.

"Baada ya kupata ushindi dhidi ya JKT Tanzania, sasa tunaendelea na maandalizi ya mechi yetu dhidi ya Dodoma jijini kuhakikisha tunapata ushindi na kufikia malengo yetu," alisema Vivier.

Azam ambayo ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi zake 50 zilizotokana na michezo 26, keshokutwa, Alhamisi itashuka katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuvaana na Dodoma Jiji FC kwenye mwendelezo wa ligi hiyo.

Habari Kubwa