Badru kubakia Mtibwa Sugar

30Jul 2021
Saada Akida
Nipashe
Badru kubakia Mtibwa Sugar

​​​​​​​BAADA ya kufanikiwa kuibakisha Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mohammed Badru amesema hafikirii kuondoka ndani ya kikosi hicho na hivi karibuni anajiandaa kufanya mazungumzo ya kusaini mkataba mpya, imefahamika.

Mohammed Badru.

Badru aliliambia gazeti hili anatarajia kukabidhi ripoti yake ya benchi la ufundi kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kuelekea katika msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo alisema analazimika kufanya mazungumzo mapya baada ya makubaliano ya awali ambayo alisaini mkataba mfupi yamemalizika na hivyo anatakiwa kupewa mkataba mpya ambao utamfanya akae klabuni hapo kuelekea msimu ujao.

"Kwa sasa niko huru, lakini uongozi wa Mtibwa Sugar umeonyesha nia ya kutaka kunipa mkataba wa kubakia ndani ya timu hii, natarajia kufanya nao mazungumzo baada ya kukabidhi ripoti yangu," alisema Badru.

Alisema anawashukuru viongozi wake kwa kusaidia kazi yake kufanyika vyema na anaamini mazungumzo yatakamilika vizuri na hatimaye kuendelea kuinoa Mtibwa Sugar baada ya kuinusuru na janga la kushuka daraja.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mtibwa Sugar, Sabri Abubakar, alithibitisha kuhusu mkataba wa kocha huyo kufikia ukingoni na hatima yake itajulikana baada ya Bodi ya Wakurugenzi kupitia ripoti yake na kutoa uamuzi.