Banda kikaangoni Simba leo

23Mar 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Banda kikaangoni Simba leo
  • Kiungo huyo anadaiwa kugoma kutekeleza maagizo ya kocha Jackson Mayanja wakati wa mechi yao ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union Jumamosi.

WAKATI Abdi Banda amedai kuwa kocha mkuu wa muda wa Simba, Jackson Mayanja "ni tatizo", uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi umesema utatoa tamko leo kuhusu utovu wa nidhamu unaodaiwa kufanywa na kiungo huyo hivi karibuni.

Jackson Mayanja.

Mayanja amedai kuwa katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara waliyoshinda 2-0 dhidi ya Coastal Union, alimtaka kiungo huyo kupasha misuli moto ili aingie uwanjani kuchukua nafasi ya beki wa pembeni kushoto, Mohamed Hussein 'Tshabalala', lakini "aligoma."

Tshabalala alionekana kuyumba katika nusu saa ya kwanza ya mchezo huo, kabla ya kuzinduka dakika tisa baadaye alipomimina krosi ya mguu wa kushoto iliyotua kichwani kwa straika Danny Lyanga na kuzaa bao la kwanza la Simba.

"Mimi ninatilia mkazo kwenye nidhamu," Mganda huyo alisema jana. "Hakuna mchezaji aliye mkubwa kuliko klabu. Unamwambia mchezaji apashe anakataa. Siwezi kulea tabia hiyo chafu."

Kutokana na msimamo wake katika kusimamia nidhamu ya wachezaji kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar na Coastal Unioni, ameamua kulifikisha suala hilo kwa uongozi wa Simba, kama ilivyokuwa kwa Hassan Isihaka anayetumikia adhabu ya kusimamishwa kwa mwezi mmoja, kulipwa nusu mshahara na kuvuliwa unahodha.

Msemaji wa Simba, Haji Manara, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa suala hilo litatolewa tamko na uongozi wa klabu hiyo leo.

BANDA ANENA
Wakati taratibu za Simba zinazuia wachezaji wa klabu hiyo kutoa taarifa kwa vyombo vya habari pasi na idhini ya klabu, Banda, mchezaji wa zamani wa Coastal Union, alitupia ujumbe kwenye moja ya mitandao ya kijamii jana akimponda Mayanja.

Banda alidai tangu Mayanja atue Msimbazi, kumekuwa na matatizo mengi kati yake na wachezaji huku akimuonya kocha huyo kuwa "kisu kitamgeukia maana malipo hapahapa duniani".

Kiungo huyo ambaye alitolewa kwa kadi ya pili ya njano katika kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga mwezi uliopita, anakuwa mchezaji wa tatu wa Simba kufikishwa mbele ya uongozi na Mayanga tangu Januari 10 Mganda huyo alipopewa mikoba ya kuinoa timu ya mabingwa hao mara 18 wa Tanzania Bara.

Alianza na Isihaka kabla ya kuuagiza uongozi wa Simba kumpa barua ya onyo straika anayetisha kwa mabao msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Hamisi Kiiza aliyetupia lawama Mganda mwenzake huo kwa kuagiza Isihaka aadhibiwe.

Licha ya migogoro hiyo na wachezaji wake, Simba chini ya Mayanja imefanya vizuri katika mechi za mashindano yote ikishinda mechi 10 kati ya 11 za Ligi Kuu na kushinda mecho zote mbili za raundi ya tatu na ya nne za Kombe la Shirikisho.

Simba kwa sasa inaongoza msimamo wa ligi ya Bara ikiwa na mtaji wa pointi 57 baada ya mechi 24, pointi saba mbele ya wapinzani wake katika mbio za ubingwa Yanga na Azam FC wanaoshika nafasi za pili na tatu baada ya mechi 21.

Imeandikwa na Renatha Msungu na Sanula Athanas

Habari Kubwa