Banka afunguka kasi ya kutupia

09Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Banka afunguka kasi ya kutupia

WAKATI akitarajiwa kuibeba tena timu yake itakaposhuka dimbani dhidi ya Mtibwa Sugar leo, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mohamed Issa 'Banka', ametoa siri ya kuendelea kucheka na nyavu.

Banka amefunga mfululizo wakati huu akitokea chumba cha majeruhi, ambapo kabla ya juzi kutupia dhidi ya Jamhuri kwenye mechi ya Kombe la Mapinduzi, pia alifunga dhidi ya Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Katika mechi hiyo ya juzi iliyopigwa Uwanja wa Amaan na Yanga kushinda 2-0, Banka alitokea benchi kipindi cha pili na kutupia dakika ya 85 baada ya Adeyum Saleh kutangulia kuziona nyavu dakika ya 45.

Akizungumza na Nipashe visiwani hapa, Banka alisema huu ni wakati wa mashabiki wa Yanga kufurahia matunda yake baada ya kumvumilia kipindi akiwa majeruhi.

"Siri kubwa ya mafanikio haya ni mazoezi na kujituma, lakini pia ushirikiano mkubwa ninaopata kutoka kwa wachezaji wenzangu.
"Nawaomba mashabiki wa Yanga waendelee kutuunga mkono watafurahia ubora wetu katika mechi zinazofuata," Banka alisema.

Akiuzungumzia mchezo wa nusu fainali leo dhidi ya Mtibwa Sugar, alisema utakuwa mgumu kwa kuwa ni timu inayowafahamu vizuri.

"Mtibwa tunacheza nao ligi moja na ni timu bora, hautakuwa mchezo mwepesi, lakini tumekuja kupambana," alisema.

Habari Kubwa