Barthez asota benchi kwa siku 102 Yanga

09Feb 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Barthez asota benchi kwa siku 102 Yanga

COASTAL Union na Prisons zimemponza Dida! Kama ilivyotarajiwa, benchi la Yanga sasa linamhusu kipa Deogratius Munishi 'Dida' baada ya kuruhusu mabao manne katika mechi mbili ambazo Wanajangwani waliambulia pointi moja wakichapwa 2-0 jijini Tanga kabla ya sare ya 2-2 mjini Mbeya.

Barthez

Kipigo dhidi ya Coastal Union ambacho kilikuwa cha kwanza kwa Yanga msimu huu, kilifuta ndondo za kipa huyo wa zamani wa Simba na Azam FC kutoruhusu nyavu za timu yake kutikiswa kwenye mechi ya nane mfululizo. Magoli mawili ya vichwa vya Jeremia Juma na mbaya wa Simba, Mohamed Mkopi yalitosha kuishusha heshima ya Dida huku kocha wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali 'Mensah' akimkumbuka Barthez ambaye benchi la Yanga lilikuwa limemzoea. Barthez alidaka mechi nane za mwanzo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu wakishinda sita na kutoka sare mara mbili huku kipa huyo wa zamani wa Simba akifungwa magoli manne. Kuchemsha kwa Dida dhidi ya Coastal na Prisons kumemrejesha Barthez kikosi cha kwanza baada ya kusugua benchi kwa siku 102 tangu Oktoba 28 alipofungwa mara mbili katika sare ya 2-2 dhidi ya Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Dida amekaa kikosi kwenye kikosi cha Yanga kwa siku 96 tangu Oktoba 31 alipocheza mechi yake ya kwanza msimu huu katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar mjini Tabora hadi Februari 3 alipotunguliwa mara mbili kwenye sare ya 2-2 dhidi ya Prisons. Ubora wa Dida ulimfanya Barthez akose mechi 14 za Yanga katika mashindano yote msimu huu -- tisa za VPL, nne za Kombe la Mapinduzi na moja ya Kombe la FA dhidi ya Friends Rangers.

Habari Kubwa