Beckham ataka Ronaldo abaki Manchester United

10May 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Beckham ataka Ronaldo abaki Manchester United

GWIJI wa Manchester United, David Beckham, amekiri mabadiliko yanahitajika pale Old Trafford, lakini anatumai Cristiano Ronaldo atabaki kuwa sehemu ya mipango ya 'Mashetani Wekundu' hao.

United ya Ralf Rangnick ilikutana na kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Brighton, Jumamosi na hiyo maana yake ni kwamba, wameruhusu mabao zaidi (56) msimu huu kuliko msimu wowote wa Ligi Kuu England.

Kocha wa Ajax, Erik ten Hag atachukua nafasi ya Rangnick mwishoni mwa msimu huu, lakini Mholanzi huyo atapewa kazi kubwa ya kukijenga upya kikosi, huku wachezaji wengi wakitarajiwa kuondoka.

Inasemekana kwamba Paul Pogba analengwa na majirani zao, Manchester City mkataba wake utakapomalizika Juni, huku mustakabali wa Ronaldo ukiwa haujulikani.

Ronaldo amefunga mabao tisa kati ya 13 ya mwisho ya ligi ya United katika mechi 11.

Hata hivyo, maswali yanaendelea kuhusu ushawishi wa mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid katika harakati za United.

Na Beckham anataka Ronaldo aonekane kama sehemu muhimu ya mipango ya Ten Hag msimu ujao.

"Ni wazi Cristiano ni mmoja wa wachezaji bora zaidi ya miaka 15 iliyopita, akiwa na Leo (Messi)," alisema Beckham akiiambia Sky Sports.

"Kuona akibaki ni jambo jema na ni muhimu kwa mashabiki. Ni muhimu kwake - sote tunajua ni kiasi gani Man United ina maana kwake. Bado anafanya kile anachofanya vema zaidi, kufunga mabao. Hicho ndicho anachofanya Cristiano.

"Kufanya kile anachofanya katika umri wake ni jambo la kushangaza sana, kwa hivyo ni matumaini yetu kwamba ataendelea kwa mwaka mwingine au miwili."

Beckham, ambaye alishinda mataji sita ya Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa United, pia anajua mabadiliko makubwa yanahitajika ili kubadilisha timu yake ya zamani kuwa na nguvu ya ushindani tena.

"Nadhani kuna mabadiliko ya kufanywa na mabadiliko yanayotokea, tumeona hilo," Beckham alisema.

"Imekuwa mwisho mgumu kwa msimu. Lakini ni mwisho wa msimu, nina hakika mashabiki wengi wanashukuru hilo kwa sababu umekuwa mgumu - uliojaa heka heka.”

Habari Kubwa