Beki wa Yanga akimbilia Ubelgiji

27Sep 2018
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Beki wa Yanga akimbilia Ubelgiji

BEKI tegemeo wa Rayon Sports ya Rwanda ambaye alikuwa anawindwa na Yanga ya jijini Dar es Salaam, Abdul Rwatubyaye, anajiandaa kwenda kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji, imefahamika.

Abdul Rwatubyaye.

Yanga ilianza kufanya mchakato wa kumsajili, Rwatubyaye, baada ya beki huyo kuonyesha kiwango kizuri katika mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika waliyokuwa wanashiriki.

Taarifa zilizopatikana kutoka Kigali, Rwanda zinasema kuwa beki huyo ambaye pia yuko katika kikosi cha timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi) mchakato wa safari yake uko katika hatua za mwisho na tayari klabu yake imeshatoa baraka.

"Wakala wake ni Mzungu na tayari ameshapeleka wachezaji wengine Ulaya akiwamo mpwa wa Haruna Niyonzima anayeitwa, Djihadi Bizimana ambaye sasa yuko Breven," alisema Clever Kazungu, mchambuzi na wakala wa ndani wa wachezaji wa Rwanda.

Aliongeza kuwa wanaamini kwa kufanya hivyo itasaidia kukuza kiwango cha timu yao ya taifa na vile vile ushindani kwenye ligi yao utaongezeka kwa wachezaji kutaka kutangaza vipaji vyao.

“Nia yetu sasa ni kupeleka wachezaji wengi vijana Ulaya, wapo wengine wawili wameshaenda Tunisia ambao wana umri chini ya miaka 20," aliongeza Kazungu.

Hata hivyo Yanga ilishindwa kuweka wazi mchakato wa kumsajili beki huyo kutokana na hali mbaya ya ukata ambayo inawakabili kwa sasa na kuishia kupiga naye picha.

Habari Kubwa