Tukio hilo lililoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki waliojitokeza kutazama mechi hiyo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, lilitanguliwa na matukio mengine mengi ikiwemo mapokezi ya wateja wa benki hiyo kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini walioshinda katika Droo ya Jaza Kibubu Na NBC.
Washindi hao walipata fursa ya kushuhudia mechi hiyo wakiwa wamelipiwa gharama zote ikiwemo za usafiri, malazi sambamba na kukatiwa tiketi za VIP kwa ajili ya kushuhudia mtanange huo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana.
Pamoja na washindi hao benki hiyo pia iliandaa mwaliko rasmi kwa ajili ya wateja wake mashuhuri wakiwemo viongozi waandamizi kutoka mashirika na taasisi mbalimbali pamoja na wadau wengine wa benki hiyo waliopata wasaa kupata chakula cha mchana pamoja na viongozi wa benki hiyo kisha kwa pamoja walielekea Uwanja wa Taifa kushudia mechi hiyo wakiwa katika msafara maalum.
Aidha, mashabiki waliojitokeza kutazama mechi hiyo walipata fursa ya kupata huduma mbalimbali za kifedha kutoka benki ya NBC kupitia maofisa wake mbalimbali waliokuwa wakitoa huduma hizo kwenye viunga vya vya uwanja huo, hatua iliyotoa fursa kwa mamia ya mashabiki hao kujiunga na huduma za benki hiyo ikiwemo kufungua akaunti mbalimbali pamoja na kufanya mihamala ya kifedha wakiwa maeneo hayo.