Benki ya Exim yatangaza wa5 wakuishangilia Stars Afcon

12Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR
Nipashe
Benki ya Exim yatangaza wa5 wakuishangilia Stars Afcon

Benki ya Exim imetangaza washindi wake watano watakaoungana na Watanzania wengine kwenda kuishangilia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ katika mashindano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon) 2019 nchini Misri.

Meneja Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Abdulrahman Nkondo (katikati), akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza washindi wa kampeni maalum ya benki hiyo inayofahamika kama “Deposit & Win – Twende Tukaliamshe Misri” watakaoungana na Watanzania wengine kwenda kuishangilia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ katika mashindano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon) 2019 nchini Misri. Washindi hao walipatikana kupitia droo kubwa ya kampeni hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Wengine pichani ni Msimamizi Mkuu wa Matawi Wateja wa Rejareja wa benki hiyo, Mwinyimkuu Ngaliama (Kulia) pamoja na Mkaguzi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Abdallah Hemedy. MPIGAPICHA WETU

Katika kampeni hiyo maalum iyofahamika kama “Deposit & Win – Twende Tukaliamshe Misri” ilikuwa inatoa fursa kwa wateja wa benki hiyo kulipiwa gharama zote za safari na malazi, ili waweze kushuhudia mechi za Taifa Stars katika mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu.

Washindi waliotangazwa jana ni Musa Mohamed kutoka Mtwara, Athumani Hassani (Manyara), Deogratius Kessy (Arusha), Msimu Ngaruka (Dar es Salaam) pamoja na Justine Tembo wa Arusha ambao wamepatikana kupitia droo kubwa ya kampeni hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam mapema jana chini ya uangalizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).

Kwa mantiki hiyo, washindi hao watano wataanza kuishuhudia Stars ikicheza mechi yake ya kwanza ya Kundi C dhidi ya Segenal Juni 23, halafu dhidi ya Kenya Juni 27 na kisha itakapoivaa Algeria Julai Mosi, mwaka huu.

Akizungumza baada ya kupatikana kwa washindi hao Mkuu wa Huduma ya Rejareja wa benki hiyo, Andrew Lyimo, alisema washindi hao watapata fursa ya kuungana na Taifa Stars katika mashindano ya Afcon nchini Misri, huku wakiwa wamelipiwa gharama zote za safari ikiwamo visa, tiketi ya ndege, gharama za tiketi ya kushuhudia mechi hizo pamoja na fedha za kujikimu.

Kwa mujibu wa Lyimo ili kushiriki katika kampeni hiyo, wateja wapya walipaswa kufungua akaunti ya akiba na kuhakikisha kila mwezi ina kiasi kisichopungua Sh. 500,000 au zaidi au kufungua akaunti ya current/biashara ikiwa na wastani wa kila mwezi wa Sh. milioni 10 au hifadhi ya amana maalum (Fixed deposit) yenye thamani isiyopungua Sh. milioni tano.

“Kwa wateja ambao tayari wana akaunti ya Benki ya Exim walichotakiwa kufanya ni kuongeza akiba kwa kiasi cha Sh. 500,000 au zaidi kwa akaunti za akiba au kuongeza kiasi cha Sh. milioni 10 kwenye akaunti zao za Current/biashara au kuwa na hifadhi ya amana maalum (Fixed deposit) yenye thamani isiyopungua Sh. milioni tano,’’ alibainisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, Stanley Kafu, alisema kampeni hiyo inatoa nafasi kwa washindi hao kuweza kushuhudia Taifa Stars ikitimiza ndoto zake za kushiriki katika mashindano ya Afcon baada ya miaka 39 kupita.

Kafu alisema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa kibenki katika kutafuta kesho bora kwa wateja wake na jamii kwa ujumla ambapo pamoja na mambo mengine benki hiyo imekuwa ikiunga mkono agenda za kitaifa ikiwsmo suala zima la michezo.

 

Habari Kubwa