BFT bado walilia kocha wa kigeni

21Feb 2016
Dar
Nipashe Jumapili
BFT bado walilia kocha wa kigeni

WAKATI Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema hakuna sababu ya kuajiri makocha wa kigeni, Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), limesema Tanzania hakuna kocha mwenye sifa za kuwanoa mabondia wa timu ya Taifa.

Waziri Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

BFT imekuwa ikililia kocha wa kigeni mwenye viwango vinavyokubalika na Shirikisho la mchezo huo duniani (AIBA) ili aweze kuwafundisha mabondia wanaojiandaa kwenda Cameroon kushiriki mapambano ya kusaka tiketi ya kushiriki michezo ya Olimpiki inayotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu.

Katibu mkuu wa BFT, Makore Mashaga alisema jana bado wanaendelea kuikumbusha Serikali kuhusu ombi lao kwa vile wanaamini ili mabondia hao waweze kufanya vizuri wanahitaji kuwa na kocha mwenye sifa.

"Kwa muda mrefu hatuna kocha mwenye viwango vya kimataifa, hili ni tatizo kubwa kwetu,” alisema na kuongeza: “Tunalazimika kuwaomba kocha majirani zetu wa Kenya kwa vile wao wana viwango.”

Waziri Mkuu Majaliwa katika risala yake kwa viongozi wa vyama vya michezo aliwataka kuondoa dhana ya makocha wa kigeni ndiyo wanaofaa kuziongoza timu za Taifa.

Aliwataka viongozi kuwa wabunifu na kutumia makocha wazalendo wenye ujuzi kuwafundisha wachezaji kwa sababu mafanikio yanaweza kupatikana bila ya timu kuongozwa na kocha wa kigeni.

Habari Kubwa