Biashara United yenye rekodi nzuri inapocheza kwenye Uwanja wa Karume Mjini Musoma ilikubali kulala bao 1-0 dhidi ya Simba wiki iliyopita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mangalu alisema mabeki wa timu hiyo hawakuwa makini katika mchezo huo, ambapo iliwaruhusu Simba kuondoka na pointi tatu.
Mangalu alisema wanashukuru makosa hayo yamemalizika na sasa wanadhamiria kuendelea kupata matokeo chanya katika mechi zinazofuata za ligi hiyo ambayo iko kwenye hatua ya lala salama.
"Leo (jana), sijafanya mazoezi, nilipata tatizo, lakini nina imani nitarudi uwanjani mapema, wachezaji wenzangu wanaendelea kujifua kwa sababu tumeweka malengo ya kumaliza msimu katika nafasi za juu, tunaamini tutafanikiwa kutimiza ndoto zetu," alisema Mangalu.
Aliongeza wachezaji wamedhamiria kuendelea kupambana katika mechi zote zilizobakia na wanaamini watapeperusha vizuri bendera ya mkoa wao.
Alisema pia wanawashukuru mashabiki wao kwa kuendelea kuwapa 'sapoti' katika kila mechi wanayocheza nyumbani na wasichoke kuwaombea kuvuna pointi tatu kwenye michezo ijayo.