Biashara United itaogopewa Bara

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Biashara United itaogopewa Bara

BAADA ya kuanza na ushindi mnono katika mechi yake ya kwanza, Kocha Mpya wa Biashara United, Amri Saidi, amesema kuwa timu hiyo itaimarika na itaonyesha ushindani katika mzungumzo wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Mpya wa Biashara United, Amri Saidi

Amri, kocha wa zamani wa Lipuli FC, alianza na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City na kufikisha pointi 13 na kuondoka mkiani katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20 za hapa nchini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Amri, alisema kuwa anaamini wachezaji wake watabadilika na kurejea katika mapambano kwenye hatua ya lala salama ya ligi hiyo.

Kocha huyo alisema kuwa aliifahamu Biashara United kabla ya kufikia uamuzi wa kutua klabuni hapo, na anachohitaji ni umoja na ushirikiano kutoka kwa wadau wa timu hiyo.

Kikosi cha Biashara United sasa kinajiandaa kuwakabili Singida United ambao watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 kutoka kwa Coastal Union.

Yanga ambayo kikosi chake cha kwanza kimebaki jijini kujiandaa na mechi dhidi ya Azam FC, ndio vinara wa ligi hiyo wakiwa na pointi 50 wakati mabingwa watetezi, Simba wenye mechi nne za viporo wakiwa katika nafasi ya tatu.

 

Habari Kubwa