Biashara United yaikatalia Simba

30Jul 2021
Saada Akida
Nipashe
Biashara United yaikatalia Simba

UONGOZI wa Biashara United umesema hauna taarifa ya nyota wao, Abdulmajid Mangalo kuondoka ndani ya timu hiyo kwa sababu bado yuko kwenye mipango yao kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.

Abdulmajid Mangalo.

Mangalo anahusishwa kutakiwa na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba kwa ajili ya msimu ujao huku beki wa Wekundu wa Msimbazi, Ame Ibrahim akihusishwa na mpango wa kutua kwa mkopo katika kikosi cha Biashara United.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Biashara United, Selemani Mataso alisema hana taarifa zozote kuhusu nyota wao Mangalo kutakiwa na Simba kwa sababu yuko katika mipango ya benchi la ufundi kuelekea msimu ujao wa ligi na mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.

"Tunahitaji kuimarisha kikosi cha timu yetu, tumekutana na kocha mkuu ameweka wazi mipango yake, kuhusu Mangalo bado tunahitaji huduma yake, sijui hao wachezaji wengi ambao wanahusishwa kutakiwa na sisi," alisema Mataso.

Kiongozi huyo alisema wamefanya kikao na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Odhiambo kwa ajili ya kukabidhi ripoti rasmi ya kikosi chao pamoja na mikakati kuelekea msimu ujao.

Aliongeza malengo yao makubwa ni kuhakikisha wanakuwa na kikosi imara kwa kutekeleza mapendekezo yatakayotolewa na Odhiambo kuelekea msimu ujao ili kujiandaa kufanya vizuri zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.