Biashara yatamba kuendeleza 'dozi'

23May 2020
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Biashara yatamba kuendeleza 'dozi'

WAKATI imefurahia uamuzi wa kurejesha Ligi Kuu Bara, uongozi wa Biashara United wamesema wamejipanga kusaka matokeo mazuri kama walivyokuwa wanashinda kabla ya ligi hiyo kusimamishwa kutokana na ugonjwa wa COVID-19.

Ofisa Habari wa Biashara United, Shomari Bhinda, alisema wameipokea taarifa ya Rais Dk. John Magufuli ya kufungua michezo kwa unyeyekevu na mikono mawili na tayari wamewaita wachezaji kwa ajili ya kuanza rasmi mazoezi ya pamoja.

"Kwanza tunampongeza Rais (JPM), kwa kuruhusu tena michezo, lakini sisi kama Biashara tumejipanga kisawasawa. Tumejipanga kuendeleza 'dozi' kama tulivyokuwa tukifanya kabla ya ligi haijasimamishwa. Si unajua kuwa wakati huo tulikuwa bora kabisa," alisema Bhinda.

Alisema kuwa wachezaji wao wote wako hapa nchini, ikiwamo wale wa kimataifa, hivyo wataingia uwanjani wakiwa na kikosi kilichokamilika.

Katika mechi tano za mwisho, Biashara United yenye pointi 40 na katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa kwenye nafasi ya 10, ilishinda mechi mbili, sare mbili na kufungwa moja.

Habari Kubwa