Biashara yawapongeza Simba, yaitahadharisha

14Feb 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Biashara yawapongeza Simba, yaitahadharisha

KOCHA Mkuu wa Biashara United, Mkenya Francis Baraza, amesema kwa sasa Simba imejiwekea heshima kubwa katika soka la Afrika baada ya kufanikiwa kupata pointi tatu muhimu katika mchezo wa kwanza wa ugenini katika hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba inayonolewa na Mfaransa Didier Gomes ilifanikiwa kuvuna pointi tatu muhimu baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji AS Vita Clu katika mechi ya Kundi A iliyofanyika juzi jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Chris Mugalu akifunga goli hilo pekee kwa penalti dakika 60 ya mchezo huo.

Kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kinatarajia kurejea nchini keshokutwa na itasafiri kuelekea mkoani Mara kuwafuata Biashara United katika mechi yake ya ligi itakayochezwa Februari 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Karume mjini Musoma.

Akizungumza na gazeti hili jana, Baraza alisema amefanikiwa kuufatilia mchezo huo kwa umakini na kuona jinsi Simba ilivyocheza kwa nidhamu ya hali ya juu na uwezo mkubwa wa kutafuta matokeo na kufanikiwa kuyapata.

Baraza alisema kitendo walichokifanya Simba katika mchezo huo wa kimataifa kimewapandisha 'daraja' na kuwaamsha wapinzani wao kujipanga zaidi wanapokutana na wawakilishi hao wa Tanzania.

"Haya matokeo na mpira ambao wamecheza Simba, nina imani kuna kitu wamekijenga kwa Afrika, ukiangalia katika mchezo dhidi ya AS Vita, Kocha Ibenge (Jean Florent), alitumia mshambuliaji mmoja hii ilionyesha jinsi gani ambavyo waliingia kwa kuwaogopa wapinzani wao, kwa kutumia mshambuliaji mmoja,” alisema Baraza.

Kocha huyo alisema Simba kupata pointi tatu ugenini ni jambo 'kubwa sana' na imejiweka katika moja ya timu zinazojadiliwa na kutengeneza kitu kwa wapinzani ambao wanakuja kukutana nao hivi karibuni kwenye Uwanja wa Benjamina Mkapa.

"Kwa upande wangu nimejipanga , tunatarajia kukutana na Simba baada ya kurejea kutoka DRC wanakuja nyumbani (Musoma), tunacheza nao, kwa jinsi nilivyowaona tunaendelea kujipanga zaidi, kuhakikisha tunapambana nao kupata matokeo chanya," alisema Baraza.

Aliongeza kila mechi huwa na mipango yake hivyo anaamini mbinu alizowapatia wachezaji wake zitasaidia kusaka matokeo chanya katika mchezo huo.

"Tunajua siku zote hakuna mechi rahisi, tutaikabili Simba kulingana na watakavyokuwa siku hiyo, hakuna mechi ndogo au kubwa katika dunia ya sasa, tutajituma na tunaamini lolote linaweza kutokea tutakavyokutana," Baraza alisema.

Habari Kubwa