Blagnon wa Simba atimkia Uarabuni

16Jan 2017
Mahmoud Zubeiry
Dar es Salaam
Nipashe
Blagnon wa Simba atimkia Uarabuni
  • ***Viongozi Msimbazi wakiri, timu ikielekea Morogoro huku...

MSHAMBULIAJI wa Simba raia wa Ivory Coast, Fredrick Blagnon jana ameondoka Dar es Salaam kwenda Oman kupitia kwao Ivory Coast kwa ajili ya mipango ya kujiunga na Fanja ya nchini humo.

Habari ambazo Nipashe ilizipata kutoka Simba jana zinaeleza kuwa Blagnon anakwenda kwao, Ivory Coast kushughulikia visa haraka ili aende Oman kufanyiwa vipimo vya afya tayari kujiunga na Fanja.

Alipoulizwa Katibu wa Simba, Patrick Kahemele juu ya safari hiyo ya Blagnon, alisema: “Ni kweli kaondoka kwa ajili ya mipango ya kwenda kujiunga na timu moja ya Oman, bado hatujaijua. Atapitia kwao, baadaye atakwenda Ivory Coast.”

Blagnon aliyekuwa analipwa zaidi Simba, dola za Kimarekani 3,000 (zaidi ya Sh. milioni sita) kwa mwezi, alijiunga na Simba Julai mwaka jana kutoka African Sports ya kwao kwa dau la Sh. milioni 100, ambazo zilitolewa na mfanyabiashara Mohamed Dewji anayetaka kununua hisa kwenye klabu hiyo.

Hata hivyo, pamoja na kusajiliwa kwa dau kubwa na kulipwa mshahara mkubwa, mchezaji huyo ameshindwa kung’ara kwenye kikosi cha timu hiyo na Simba imeridhia mpango wa kumuuza Oman.

Simba ilikiimarisha kikosi chake kwenye dirisha dogo la usajili kwa kumsajili mshambuliaji wa Zesco ya Zambia, Mtanzania Juma Luizio ambaye ujio wake umeonekana kumyima nafasi Balgnon kwenye kikosi cha kwanza.

Mbali na Luizio, Simba pia ilimsajili mshambuliaji wa Stand United, Pastory Athanas ambaye naye amekuwa chaguo la mara kwa mara la Kocha Joseph Omog.

Wakati huo huo: Kikosi cha Simba kimeondoka jana mchana mjini Dar es Salaam kwenda Morogoro tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji Mtibwa Sugar Jumatano.

Habari Kubwa