BMT mguu sawa kutumbuliwa majipu

12Feb 2016
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
BMT mguu sawa kutumbuliwa majipu

WIKI moja imepita tangu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuwasimamisha kazi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo na msaidizi wake, Juliana Yasoda.

Kazi hiyo ya kusafisha watendaji wa Serikali iliyopewa jina la 'Tumbua majipu', haijaishia kwa viongozi hao tu, bali inaendelea katika sekta yote ya michezo, imefahamika mwishoni mwa wiki hii.

Akizungumza na Nipashe jana, Nnauye alisema kwa sasa uchunguzi dhidi ya viongozi hao waliosimamishwa bado unaendelea.

"Viongozi hawa wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi, hatujawafukuza kama wengi wanavyofikiria," alisema Nnauye.

Alisema kinachofanyika sasa ni kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili na baada ya hapo tutafahamu nini kitaendelea.

"Uamuzi wa serikali utategemea na majibu ya uchunguzi unaoendelea kufanyika," alisema waziri huyo bila kufafanua ni lini uchunguzi huo utakamilika.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa wizarani hapo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwenye gazeti kwa kuwa siyo msemaji, alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kusafisha watendaji wote walioshindwa kuwajibika kwenye nafasi zao na sasa wanahamia BMT.

"Baada ya kumaliza kuweka sawa kule BMT, tutafahamu nani atachukua nafasi ya Thadeo na Yasoda," alisema mtoa habari huyo.

Alisema viongozi waliosamishwa na wale watakaosimamishwa ni wale walioshindwa kuwajibika ipasavyo.

Thadeo na Yasoda ni viongozi wa kwanza wakubwa katika sekta ya michezo kusimamishwa kazi tangu Rais John Magufuli aingie Ikulu.

Wakati huohuo, Nnauye kesho atafanya ziara ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikiwa ni mara ya kwanza tangu ashike wadhifa huo.

Habari Kubwa