Bocco aahidi Simba kuendeleza ushindi

23Mar 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Bocco aahidi Simba kuendeleza ushindi

NAHODHA wa Simba, John Bocco, amesema licha ya jukumu walilonalo la kuipeperusha bendera ya Taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kikosi cha timu hiyo hakitaacha "kitu" kwenye michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba ina viporo saba vya Ligi Kuu Bara ambavyo vimetokana na kuwa na jukumu la michuano ya kimataifa wanayoshiriki na sasa wametinga hatua ya robo fainali.

Akizungumza na gazeti hili, Bocco ambaye yupo katika kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), alisema kuwa bado wanafahamu jukumu la kufanya vema katika Ligi Kuu na wataendelea kupambana ili kushinda mechi zote zilizobakia msimu huu.

“Michezo ya kimataifa tuliyofanya vizuri imetupa molari na hamasa ya kutaka kuona tunatetea ubingwa wetu, hii ndio sababu tunakuwa makini katika michezo yetu ya Ligi Kuu, kila mmoja wetu anataka kuona hatupotezi mchezo wowote ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa,” alisema Bocco.

Kuhusu mchezo wao na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Bocco alisema wanafahamu timu ni kubwa hapa barani Afrika yenye wachezaji wenye uzoefu wa michuano hiyo.

“Tunawaheshimu kwa jambo hilo kwa sababu wameshatwaa ubingwa wa michuano hii, lakini na sisi tuna timu nzuri, tutapambana katika mechi zote mbili ili kuhakikisha tunasonga mbele,” Bocco alisema.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walisonga mbele katika michuano hiyo baada ya kuifunga AS Vita ya DRC na kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi D lililoongozwa na Al Ahly ya Simba.

Habari Kubwa