Bocco afikisha magoli 10 Azam FC vs Yanga

07Mar 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Bocco afikisha magoli 10 Azam FC vs Yanga
  • Straika huyo ambaye hajawahi kuihama Azam FC tangu aipandishe Ligi Kuu msimu wa 2008/09, amezoea kuwatungua Wanajangwani.

MSHAMBULIAJI na Nahodha wa wa Azam FC, John Bocco 'Adenayor', amefikisha magoli 10 kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara za timu yake dhidi ya Yanga tangu msimu wa 2008/09 uliokuwa wa kwanza kwa Wanalambalamba Ligi Kuu.

John Bocco 'Adenayor

Mchezaji huyo alifunga bao la pili kwenye mechi ya juzi wakati Azam FC ikitoka sare ya 2-2 dhidi ya mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo kubwa zaidi nchini.

Bocco ndiye mchezaji aliyefunga magoli mengi zaidi tangu katika mechi za timu hizo tangu zianze kupambana Ligi Kuu.

Alianza kufunga goli lake la kwanza msimu wa 2009/10 Azam FC ilipotoka sare ya bao 1-1, goli lingine lilikuwa ni la kufutia machozi timu hiyo cha Chamazi ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 kwenye mechi ya mzunguko wa pili msimu huo.

Bocco alifunga bao la tatu msimu wa 2010/11 likiwa goli pekee na la nne alilipata kwenye mechi ya mzunguko wa pili msimu huohuo Azam ikichapwa mabao 2-1.

Msimu wa 2011/12 alifunga bao pekee, Azam ikiichapa Yanga bao 1-0 na kuwa bao lake la tano, kabla ya kufunga magoli mawili msimu huohuo katika mechi ya mzuguko wa pili Azam ikiisasambua Yanga mabao 3-1 na kuwa bao lake la saba.

Alifunga goli moja na la nane kwake msimu 2013/14 timu yake ikiiadhibu Yanga mabao 3-2 na msimu wa 2014/15 alifunga bao lingine likiwa ni la kusawazisha timu hizo zilipotoka sare ya mabao 2-2 na kufikisha idadi ya magoli tisa, kabla ya juzi kufuta ndoto za Wanajangwani kutoka na ushindi kwenye Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa