Bocco arejea kuiongoza Azam

19Mar 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Bocco arejea kuiongoza Azam

MABINGWA wa mashindano ya Kombe la Kagame, Azam FC, leo wanatarajia kuwavaa Mbabane Swallows katika mechi ya marudiano ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa (Somhlolo), mjini Manzini kuanzia saa 10:30 jioni kwa saa za Tanzania.

John Bocco.

Azam FC itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Ramadhani Singano 'Messi' katika mchezo wa kwanza uliofanyika Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aristica Cioaba amesema kuwa kikosi chake kimefanya maandalizi vizuri kwa ajili ya mchezo huo na wanachosubiri ni muda wa mechi ufike huku akitarajia kumtumia nahodha wake, John Bocco.

Cioaba alisema kuwa licha ya kupata ushindi katika mechi ya kwanza, wataingia uwanjani wakiamini wanatakiwa kuanza upya 'vita' ya kusaka tiketi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Wakati huo huo, meneja wa timu hiyo, Alando, alisema kuwa kundi la kwanza la kikosi hicho liliondoka jana asubuhi kutoka Pretoria Afrika Kusini na kuelekea Swaziland tayari kwa mchezo huo.

Alitaja katika msafara huo utaongozwa na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, Saad Kawemba, James Mhagama, Herry Mzozo, Mwanandi Mwankemwa, Yusuph Nzawila, Iddi Cheche na nahodha John Bocco.

"Msafara unaofuatiwa utaongozwa na Jamal Bakhressa na kikosi chetu kitalala Manzini, wapinzani wetu wanatumia Uwanja wa Taifa (Somhololo) ambao uko nyumbani kwao Manzini, tunaomba sala na dua za Watanzania wote," alisema meneja huyo.

Mabingwa hao wa Kombe la Kagame, wanahitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili kuweza kusonga mbele katika michuano hiyo ya kimataifa.

Habari Kubwa