Bocco azua hofu Simba usajili Sauzi

12Jun 2019
Somoe Ng'itu
DAR
Nipashe
Bocco azua hofu Simba usajili Sauzi
  • ***Ni baada ya Polokwane City ya Afrika Kusini kusema wameshamalizana, uongozi Msimbazi waja juu wasema...

FILAMU na maigizo kuhusu usajili wa wachezaji wa Tanzania umeendelea kuchukua nafasi yake kuelekea msimu mpya baada ya kuwapo na taarifa tofauti kuhusu usajili wa mshambuliaji na nahodha wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, John Bocco.

Taarifa zilizoonekana juzi sambamba na picha katika mitandao ya kijamii, zilionyesha Bocco akisaini mkataba mpya wa miaka miwili wa kuitumikia Simba, lakini jana ofisa mmoja wa Polokwane City ya Afrika Kusini ameweka wazi kwamba mshambuliaji huyo ni mali yao.

Bocco ambaye hakuwa na timu yake katika mchezo wa mwisho wa kufunga pazia dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa Morogoro, ilielezwa kwamba ni mgonjwa, alionekana akisaini mkataba mpya mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mohammed "MO" Dewji.

Kiongozi huyo wa Polokwane alisema kuwa Bocco alisaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo akiwa kama mchezaji huru baada ya kuelezwa amemaliza mkataba na Simba.

Aliongeza kuwa Polokwane City hawatakaa kuzungumza chochote na Simba kwa kuwa walimsainisha kwa sababu hakuwa na mkataba na klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alinukuliwa jana akisema kuwa wana taarifa kuwa Porokwane FC walimsajili Bocco Aprili 9, mwaka huu, wakati akiwa bado na mkataba na Simba, huku akiendelea kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara iliyomalizika Mei 28, mwaka huu.

"Unajua mchezaji anaweza kuongea na klabu na kukubaliana miezi sita kabla ya kumalizika kwa mkataba, lakini ni lazima klabu yake ijulishwe hata kama wakijibiwa au la, hawa jamaa walimsainisha bila kututaarifu wakati mchezaji ana mkataba na sisi, lakini waliposikia tumemuongeza mkataba ndiyo wakaja ofisini kusema wanamhitaji, wakati huo tayari sisi tuna taarifa zao kuwa wamemsainisha kabla." alinukuliwa Magori.

Magori alisema kuwa timu hiyo ndiyo ina makosa na kama inaona ina haki basi iende kushtaki Shirikisho la Soka duniani (Fifa).

"Bocco ni mchezaji wetu tumemuongeza mkataba wa miaka miwili, hao wanaosema wamemsajili ni batili," alisema.

Bocco alijiunga na Simba akitokea kwa mabingwa wa Kombe la FA, Azam FC na msimu uliomalizika ameisaidia timu yake kufika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa pili mfululizo.

Kabla ya kusaini Polokwane City ambayo mkataba wake unatakiwa kuanza Julai Mosi, mwaka huu, Bocco alikuwa anahusishwa na tetesi nyingine za kurejea Azam FC.

Katika tuzo za Mo mwaka jana, Bocco alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa klabu hiyo, tuzo ambayo msimu huu imechukuliwa na mshambuliaji Mnyarwanda Meddie Kagere.

Habari Kubwa