Bocco, Chama kuituliza Simba leo

26Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bocco, Chama kuituliza Simba leo

BAADA ya kuwakosa washambuliaji wake nguli katika mechi iliyopita, Kocha Mkuu wa Simba , Sven Vandenbroeck, anaweza kumtumia straika John Bocco katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting katika Uwanja wa Uhuru leo.

Lakini kiungo mnyumbulifu Clatous Chama naye atakuwa tayari kucheza baada ya kuikosa mechi iliyopita mjini Sumbawanga wakati wakichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Tanzania Prisons.

Bocco pamoja na washambuliaji wenzake Meddie Kagere na Chris Mugalu, wote walikuwa majeruhi, hivyo Sven kulazimika kumtumia Charles Ilamfya ambaye alishindwa kufurukuta ngome ya ulinzi ya Prisons Alhamisi iliyopita katika Uwanja wa Nelson Mandela.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kwa mujibu wa Daktari wa Simba, Yassin Gembe, Bocco anaweza kucheza kama atakuwa katika mipango ya mwalimu.

"Bocco amesharejea na amekuwa akifanya mazoezi na wenzake, hivyo kucheza ama kutokucheza itategemea na mipango ya kocha," alisema Manara.

Akizungumzia mchezo huo, Sven alisema amewataka wachezaji wake kusahau matokeo yaliyopita na kuelekeza akili zao kwenye mchezo wa leo.

Sven alisema walipata matokeo waliyostahili kwa sababu hawakupigania ushindi, hivyo leo hawana budi kuhakikisha wanashinda dhidi ya Ruvu Shooting.

“Tunapaswa kukubali na kusonga mbele, tayari nimewataka wachezaji wangu kutazama mechi inayofuata,” Sven alinukuliwa na tovuti ya klabu hiyo.

Habari Kubwa