Bocco: Simba kicheko Z'bar mpaka Caf

11Jan 2019
Isaac Kijoti
Zanzibar
Nipashe
Bocco: Simba kicheko Z'bar mpaka Caf

WAKATI kikosi cha wachezaji 18 cha Simba kikiondoka Zanzibar juzi kurejea Dar es Salaam, nahodha wa timu hiyo, John Bocco, hakuwa na maneno mengi zaidi ya kusema "tunaimani ya ushindi".

Bocco ambaye ni miongoni mwa wachezaji 18 waliorejea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi dhidi ya JS Saoura ya Algeria, alisema ana imani pia kwa Simba kuendeleza furaha ya ushindi Kombe la Mapinduzi.

"Wachezaji nane wa kikosi cha kwanza waliobaki Zanzibar ninaimani watashirikiana vema na wale wa Kikosi B kuendeleza ushindi.

"Kadhalika, maandalizi mazuri tuliyoyafanya, ninaamini pia tutashinda mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa," alisema nahodha huyo anayetarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji sambamba na Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.

Simba ambayo ilikuwa na jeshi lake kamili visiwani hapa, iligawa kikosi chake na kuwaacha wachezaji nane kuungana na wa Kikosi B kwa ajili ya kucheza mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi leo saa 2:15 usiku dhidi ya Malindi ambayo itatanguliwa na nusu fainali ya kwanza kati ya Azam FC na KMKM saa 10: 15.

Wachezaji nane waliobaki Zanzibar kuungana na wale wa Kikosi cha U-20 kucheza nusu fainali ni Ally Salim, Zana Coulibaly, Asante Kwasi, Paul Bukaba, Yusuph Mlipili, Mohamed Ibrahim, Abdul Seleman 
na Adam Salamba.

Kwa upande watakaobeba jukumu la kuipeperusha bendera ya Afrika Mashariki na Kati kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa  kesho Jumamosi ni Aishi Manula, Deogratius Munishi, Nicholas Gyan, Hussein Mohamed, Juuko Murshid na Pascal Wawa.

Wengine ni Jonas Mkude, James Kotei, Clatous Chama, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Said Ndemla, Mzamiru Yassin, Shiza Kichuya, Rashid Juma, John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Baada ya mechi hiyo, Simba itaifuata AS Vita ya DR Congo Januari 19 kabla ya kuhitimisha mzunguko wa kwanza wa hatua ya makundi kwa kuvaana na Al Ahly ya Misri ugenini Februari 2, mwaka huu.

Habari Kubwa