Bokungu arejea, ashukia KMC

05Jul 2019
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Bokungu arejea, ashukia KMC

BEKI wa zamani wa Klabu ya Simba Mkongomani Javier Besala Bokungu, amerejea tena nchini Tanzania na kujiunga na Klabu ya KMC inayomilikiwa na Manispaa ya Kinondoni.

Javier Besala Bokungu

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ni kwamba Bokungu amesaini mkataba wa mwaka mmoja, na amekuja pamoja na mchezaji mwingine kutoka Congo, Melly Sivirwa ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili akitokea Klabu ya Vital'O ya Burundi.

Bokungu anayemudu kucheza nafasi ya beki wa kulia na pia beki wa kati, amejiunga na KMC akitokea Klabu ya Groupe Bazano ya nchini Congo.

Hii ni mara ya pili sasa kwa mchezaji huyo kurejea nchini kwani aliichezea Simba mwaka 2016 na 2017, lakini aliondoka baada ya mkataba wake kumalizika.

Atakumbukwa kwa kuipa Simba ushindi dhidi ya mahasimu wao wa jadi kwenye Kombe la Mapinduzi hatua ya nusu fainali mwaka 2017 alifunga penalti ya nwisho, Simba ikiichapa Yanga kwa penalti 4-2.

Hata hivyo, Simba ikafungwa kwenye fainali dhidi ya Azam FC.

Kusajiliwa kwa wachezaji hao ni muendelezo wa Klabu ya KMC kuboresha kikosi chake hasa kwa wachezaji wazoefu na wa kimataifa, hususan itakapokwenda kukabiliana na timu mbalimbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kabla ya kuichezea Simba, Bokungu aliwahi kuzichezea Klabu za TP Mazembe na Esperance kwa nyakati tofauti.