Bossou wa Yanga kushuka leo uwanjani Gabon

16Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bossou wa Yanga kushuka leo uwanjani Gabon

BEKI wa Yanga, Vincent Bossou leo anatarajiwa kuanza kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, wakati timu yake,Togo itakapomenyana na mabingwa watetezi, Ivory Coast katika mchezo wa kwanza wa Kundi C huko Gabon.

BEKI wa Yanga, Vincent Bossou.

Togo na Ivory watamenyana saa 1:00 usiku Uwanja wa d'Oyem, kabla ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kumenyana na Morocco saa 4:00 usiku katika mchezo wa pili wa kundi hilo.

Bruce Kangwa wa Azam FC, jana aliiwakilisha timu yake ya Taifa ya Zimbabwe ilipomenyana na Algeria katika mchezo wa Kundi B.

Bossou ni beki tegemeo kwenye timu yake ya Taifa na tangu alipojiunga na Yanga hajaachwa kwenye timu ya Taifa.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi akizungumza na Nipashe jana, alisema uwezo wa nyota huyo utaisaidia timu yake ya taifa kufanya vizuri kwenye fainali hizo.

"Sisi tunamtakia kila la heri, ni mchezaji mzuri na tunaamini uwezo wake utaisaidia timu yake ya taifa," alisema Mwambusi.

Fainali hizo zilianza juzi jioni kwa mchezo kati ya wenyeji Gabon dhidi ya Guinea- Bissau ambapo timu hizo zilitoka sare kwa kufungana bao 1-1 na baadaye Cameroon kupata matokeo kama hayo dhidi ya Burkina Faso.

Habari Kubwa