Bravo JPM, Kenyatta kuingilia kati mipaka

22May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Bravo JPM, Kenyatta kuingilia kati mipaka

MARAIS John Magufuli wa Tanzania na Uhuru Kenyatta wa Kenya, wamesafisha hali ya hewa, kufuatia hali ya sintofahamu kwenye mipaka ya nchi hizo mbili.

Hali hiyo ilijitokeza hivi karibuni kutokana na kasoro zilizojitokeza kuhusiana na utaratibu wa kuwaruhusu madereva wa malori ya mafuta.

Kikubwa ni utaratibu wa kuwataka wapimwe kupimo cha virusi vya corona, lakini ikaonekana kuna dosari ambazo zilizua shaka kuwa huenda kuna nia mbaya ya kuzorotesha uhusiano mzuri na wa kuhistoria ambao ni wa muda mrefu kati ya mataifa haya jirani ya Afrika Mashariki.

Kwa kuliona tatizo hilo, wakuu hao wawili wa mataifa hayo, wamewaagiza mawaziri wanaohusika na uchukuzi na wakuu wa mikoa iliyoko katika pande zote za mpaka wa Tanzania na Kenya, kukutana na kutatua mgogoro uliosababisha kuzuiwa kwa malori ya mizigo kuvuka mpaka huo.

Rais Magufuli alisema hayo juzi, alipokuwa akiwasalimu wananchi wa Singida akiwa safarini kutoka Chato mkoani Geita kwenda makao makuu ya nchi jijini Dodoma.

Siku chache zilizopita umeibuka mgogoro katika vituo vya mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mikoa ya Mara, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro baada ya malori ya mizigo ya kutoka Tanzania kuzuiwa kuingia Kenya kwa madai ya madereva wanaopimwa kukutwa na maambukizo ya virusi vya corona.

Rais Magufuli alibainisha kwamba, Rais Kenyatta alimpigia simu Jumanne na Jumatano, na katika mazungumzo yao wamekubaliana kuwa viongozi wa pande zote mbili wanapaswa kukutana na kuutatua mgogoro huo haraka iwezekanavyo ili Watanzania na Wakenya waendelee kufanya biashara zao kama kawaida.

Alisema kwamba kuzuiwa kwa malori ya Tanzania yanayokwenda Kenya ama kuzuiwa kwa malori ya Kenya kuja Tanzania hakukubaliki.

Aliwataka viongozi wa pande zote mbili waweke maslahi ya Tanzania na Kenya mbele, waache kuamua mambo kwa jazba na akaagiza wakuu wa mikoa ya Mara, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert Ibuge, kuhakikisha mazungumzo hayo yanafanyika ndani ya wiki moja.

Kenya na Tanzania ni nchi ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambayo inaziwezesha nchi zote wanachama zikiwamo Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini kushirikiana katika sekta mbalimbali kama za biashara, uchumi, utalii, miundombinu na usafirishaji, kwa kutaja baadhi.

Kwa hiyo njia pekee ya kutatua changamoto zinapojitokeza ni kwa wahusika kutumia njia za mawasiliano na majadiliano ili kuweka mambo sawa kwa manufaa na ustawi wa wananchi wa jumuiya hiyo.

Tunawapongeza wakuu hao wa nchi hizo kuingilia kati kwa kutoa maelekezo kwa mawaziri na maofisa wa kila upande kukutana kwa ajili ya kurekebisha mambo.

Suala hilo linapaswa kuwa fundisho kwa viongozi na maofisa wa serikali za nchi hizo na zingine za EAC kujenga utamaduni wa kukutana na kujadiliana namna ya kumaliza changamoto zinapojitokeza kabla hazijasababisha athari zaidi kwa wananchi na nchi hizo kwa ujumla.

Mawaziri, watendaji na maofisa wengine ni wajibu wao kushughulikia na kumaliza changamoto hizo badala ya kuwaachia jukumu hilo wakuu wa nchi na serikali, ambao wana majukumu mengi na makubwa.

Ni matarajio yetu kwamba mawaziri, watendaji na maofisa wetu pia watachukua hatua kushughulikia changamoto zilizoko katika mpaka wa Tunduma, ambapo madereva kutoka nchini wanalalamikia upande wa Zambia kwa kuwanyanyasa, hivyo kutishia kuvuka na malori yao ya mizigo.

Habari Kubwa