Cannavaro si wa leo, wala kesho

16Mar 2016
Lete Raha
Cannavaro si wa leo, wala kesho

NAHODHA wa timu ya soka ya Yanga, Nadir Haroub Canavaro amesema kurejea kwake uwanjani kuendelea na kikosi cha wanajangwani hao, kutatokana na ruhusa ya Daktari ambaye anaendelea naye katika mazoezi mepesi, ili kuhakikisha anakuwa fiti.

Nadir Haroub Canavaro

Akizungumza na gazeti hili jana, Canavaro alisema kurejea katika kikosi chake, kutatokana na taarifa ya madaktari kutoka India ambao wanaendelea kumpa mazoezi na matibabu katika kliniki ya Nandal ilioko Msasani jijini Dar es Salaam.

Canavaro alisema awali ilipangwa afanyiwe operesheni kwa mara nyingine, lakini baada ya uchunguzi wa madaktari kutoka India, walisema aendelee na mazoezi mepesi, chini ya uangalizi wa madaktari hao,ambapo atarejea uwanjani wakati wowote watakapomruhusu.

"Kwa kweli naendelea vizuri, nafanya mazoezi mepesi, kwenye gym,ilio kwenye klini hiyo, chini ya madaktari jambo ambalo linanipa matumaini ya kurejea uwanjani haraka,"alisema Canavaro.

Alisema, ukiacha hilo, pia anafarijika kuona wachezaji wenzake wanapambana uwanjani, ili kuhakikisha Yanga inafanya vizuri katika mechi zake za Ligi Kuu bara na zile za Klabu Bingwa Afrika.

Alisema kutokana na hilo,amewatoa wasi wasi mashabiki wa Yanga, kuhusiana na yeye kurejea uwanjani, ambapo alisema Daktari akitoa ruhusa, atakuwa tayari kuungana na wenzake katika mechi za Ligi.

Akizungumzia ushindani kwa ujumla, alisema ligi kwa sasa inaushindani mkubwa, lakini anakiamini kikosi chao, kutokana na uwezo wa kupambana waliokuwa nao uwanjani.

Canavaro yuko nje, takribani miezi miwili sasa, baada ya kupata majeraha akiwa na timu ya taifa wakati wa mechi dhidi ya Algeria iliofanyika Septemba mwaka jana.

Habari Kubwa