Cannavaro: Tujipange kuvuka makundi

21Apr 2018
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Cannavaro: Tujipange kuvuka makundi

NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, amesema klabu hiyo sasa inatakiwa kujipanga kuhakikisha wanavuka hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.

NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro.

Yanga imefanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuitupa nje Welayta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1.

Akizungumza mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam wakitokea Ethiopia, Cannavaro, alisema kuwa litakuwa jambo la maana kama watavuka hatua hiyo waliyoshindwa kuivuka mwaka juzi.

“Mwaka 2016 tulifanikiwa kufikia mafanikio haya ya kutinga hatua ya makundi lakini hatukuvuka hapo, safari hii lazima tujipange na kuhakikisha tunajiandaa vyema ili kuvuka hatua hii, hayo yatakuwa mafanikio kwetu,” alisema Cannavaro.

Alisema mashabiki na viongozi waunganishe nguvu zao pamoja na wachezaji kujipanga vyema kuelekea kwenye michezo ya makundi.

Aidha, kuitoa klabu hiyo ya Ethiopia kumewaongezea morali wachezaji kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michezo yao ya ligi kuu.

“Sasa tunaelekeza nguvu kwenye michezo yetu ya ligi kuu, kitendo cha kutinga hatua ya makundi kitaongezea morali ya kuona tunafanya vyema kwenye michezo yetu ya ligi,” alisema Cannavaro.

Yanga inajiandaa kuumana na wapinzani wao Simba Aprili 29 kwenye uwanja wa Taifa.  

Habari Kubwa