Chama aanika kiwango chake

28Feb 2019
Somoe Ng'itu
Iringa
Nipashe
Chama aanika kiwango chake

KIUNGO wa kimataifa wa Simba kutoka Zambia, Clatous Chama, amewataka wadau wa timu hiyo wanaohoji kiwango chake pale kinapoonekana kushuka wasiwe na wasiwasi naye kwa sababu yeye ni "binadamu na si Mungu".

Chama aliifungia Simba mabao mawili katika ushindi wa 3-1 walioupata katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi mkoani hapo, huku la tatu likipachikwa nyavuni na Mnyarwanda, Meddie Kagere.

Kiwango cha Chama kilionekana kushuka kuanzia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly iliyochezwa Misri, ambapo Simba ilichapwa mabao 5-0 kutoka kwa vigogo hao.

Hata hivyo, kiungo huyo wa Timu ya Taifa ya Zambia maarufu Chipolopolo juzi, alionekana kurejea katika ubora wake na kuisaidia Simba kuvuna pointi tatu kwenye Uwanja wa CCM Samora na kuendelea na mbio zake za kutetea ubingwa wa Bara.

Chama alisema kupanda na kushuka kwa kiwango cha mchezaji ni jambo la kawaida na hiyo haitokani na mapenzi ya mchezaji ila inatokana na changamoto ya mazingira yanayomzunguka nyota husika.

"Hakuna mchezaji anayependa kucheza katika kiwango cha chini, kila siku mchezaji hujipanga kuonyesha kiwango cha juu, lakini mazingira na wakati uliopo huchangia kuonekana tofauti, hapa ni Afrika na si Ulaya, mimi bado ni Chama yule yule," alisema kiungo huyo.

Alisema analishukuru benchi la ufundi na wachezaji wenzake wa Simba kwa kuendelea kumpa ushirikiano wakati wote na hasa juzi kuaminiwa na kuchangia kufunga mabao mawili katika mchezo huo.

Baada ya mechi ya juzi, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walitimiza pointi 48 wakiwa wamecheza mechi 19 na mchezo wao unaofuata utachezwa Jumapili dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.

Habari Kubwa