Chama agawa zawadi kwa mashabiki Simba

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Chama agawa zawadi kwa mashabiki Simba

KIUNGO wa Simba, Clatous Chama, amesema bao la ushindi alilofunga juzi kwenye mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita, amelitoa kwa mashabiki wa timu hiyo ambao wamekuwa wakiwasapoti.

KIUNGO wa Simba, Clatous Chama

Chama juzi alifunga bao hilo muhimu na kuifanya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na hivyo kufuzu hatua ya robo fainali.

Chama alisema mashabiki wa Simba wamekuwa wakiwasapoti muda wote, hivyo na wao kama wachezaji wamekuwa wakipambana uwanjani ili wasiwaangushe.

"Na bao la ushindi ambalo nimefanikiwa kufunga ni maalum kwa mashabiki wa Simba na shukrani kwa kuendelea kutusapoti," alisema Chama.

Alisema kwa sasa wanaangalia mbele zaidi baada ya kufuzu hatua hiyo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Bao hilo la Chama lililowapa ushindi Simba alilifunga dakika ya 88 akikumbushia bao la ushindi kwenye mchezo wa mtoano kuwania kuingia hatua ya makundi dhidi ya Nkana ya Zambia ambayo Simba ilishinda mabao 3-1 shukrani kwa bao la dakika za mwisho la Chama.

Simba sasa inasubiri Jumatano kumjua mpinzani wake kwenye hatua ya robo fainali wakati droo itakapochezeshwa jijini Cairo, Misri.   

 

Habari Kubwa