Chama ana siri moyoni

18Oct 2020
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Chama ana siri moyoni
  • ***Kiungo huyo anayetajwa Yanga anarejea nchini leo kuendelea na majukumu...

WAKATI akiwa bado hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Simba, kiungo wa kimataifa wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutoka Zambia, Clatous Chama, amesisitiza hana mpango wowote wa kujiunga na watani zao, Yanga.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum, Chama alisema yuko katika hatua za mwisho za kukamilisha mazungumzo na Simba na anaipa nafasi kubwa klabu hiyo kwa hapa nchini.

Chama alisema amekuwa na msimu mzuri ndani ya Simba na hiyo ni moja ya sababu  inayomfanya afikirie kuongeza mkataba mpya wa kuitumikia klabu hiyo yenye makao makuu yake Mtaa wa Msimbazi Kariakoo jijini, Dar es Salaam.

Kiungo huyo alisema kwa sasa hajawahi kufikiria kujiunga na Yanga kwa sababu anafurahia maisha ndani ya kikosi cha Simba.

"Kwenda Yanga? Hapana. Ninaamini hivi karibuni nitakamilisha mchakato huo, Simba kuna raha, patamu eeee," alisema kwa kifupi nahodha huyo wa Timu ya Taifa ya Zambia (Chipolopolo).

Nyota huyo alisema anatarajia kurejea nchini leo baada ya kupata hati mpya ya kusafiria ambayo alienda kubadilisha nchini kwao.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, alisema kikosi chao kitaendelea na mazoezi yake leo asubuhi na maandalizi ya safari ya kuelekea Sumbawanga kuwafuata Tanzania Prisons yamekamilika.

Rweyemamu alisema wataondoka na wachezaji wote ambao wako tayari kwa mechi hiyo, huku majeruhi wakiendelea na programu maalumu za mazoezi chini ya mwongozo wa daktari wao, Yasin Gembe.

Alisema Tanzania Prisons ni moja ya timu zenye vikosi imara na kupata matokeo mazuri inatakiwa kujipanga na kuongeza umakini.

"Tutaondoka Jumatatu na kwenda kupumzika Mbeya, kesho yake (Jumanne), ndio safari ya kwenda Sumbawanga itaanza, tunajua huko tunakwenda kukutana na timu inayotoa changamoto, hatutabweteka, ni mechi itakayokuwa na ushindani," Rweyemamu alisema.

Aliongeza ushindani katika kikosi cha Simba unaongezeka kila siku kwa sababu kila mchezaji anahitaji kuwa sehemu ya wachezaji 18 ambao Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck anawaamini kuelekea mchezo husika.

Aliwataka mashabiki na wanachama wa Simba kuendelea kushirikiana na viongozi ili kufikia malengo ya timu kwa sababu msimu huu ni mgumu zaidi.

"Kuchukua ubingwa wa ligi mara tatu mfululizo si jambo dogo, timu zote 17 zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara zinatuangalia sisi, sio kwa sababu tuna kikosi kizuri, zinataka kutupa changamoto mabingwa watetezi, tunalijua hilo, tumejipanga vizuri kutetea taji," alisema meneja huyo.

Tanzania Prisons iliyohamia kwenye Uwanja wa Nelson Mandela msimu huu, itaikaribisha Simba katika mechi ya raundi ya sita itakayofanyika Jumatano kuanzia saa 10:00 jioni, huku siku hiyo hiyo Yanga ikikutana na 'Maafande' wa Polisi saa 1:00 usiku.

Azam FC yenye pointi 18 baada ya kushinda mechi zake zote sita, ndio vinara wa ligi hiyo wakifuatiwa na Simba, Yanga na Biashara United zenye pointi 13 kila moja.

Habari Kubwa