Chama awatuliza mashabiki Simba

20Mar 2019
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Chama awatuliza mashabiki Simba
  • ***Ni wakati droo ya robo fainali Caf ikipangwa leo, asema hata wakija Esperance...

KIUNGO wa Simba, Clatous Chama, amesema hawana hofu na timu yoyote watakayopangwa nayo kucheza hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati droo ya hatua hiyo itakapochezeshwa leo jijini Cairo, Misri.

Akizungumza na Nipashe jana, Chama, alisema kwa hatua waliyofikia kwa sasa ni vita na wapo tayari kukabiliana na timu yoyote.

"Tutajipanga, kufika hatua hii tumefanya kazi kubwa na bado tuna kazi mbele yetu, hatujui tutacheza na nani, lakini tupo tayari kukabiliana na timu yotote," alisema Chama.

Nyota huyo ambaye alifunga bao la ushindi kwenye mchezo dhidi ya AS Vita walioibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutinga robo fainali, alisema kila timu iliyotinga hatua hiyo ni bora.

"Kila mchezo una mipango yake, baada ya droo kocha atapanga nini cha kufanya kuhakikisha tunaingia hatua inayofuata," alisema Chama.

Mbali na Simba, timu nyingine zilizotinga hatua hiyo ni Esperance ya Tunisia, Wydad Casablanca ya Morocco, TP Mazembe ya Congo, Mamelod ya Afrika Kusini, Horoya ya Guinea, Asec Mimosa ya Ivory Coast na Al Ahly ya Misri.

Hata hivyo, uwezekano mkubwa upo kwa Simba kukutana na Esperance, Wydad Casablanca ama TP Mazembe.

Simba imefika robo fainali baada ya kuanzia hatua ya awali ya michuano hiyo kwa kuichapa Mbambane Swallow ya Swaziland kwa sasa Eswatini, kwa mabao 4-1 Uwanja wa Taifa kabla ya kwenda kwao na kuifumua 4-0, na kusonga mbele kwa jumla ya tofauti ya mabao 8-1.

Katika mechi ya mtoano, kuwania kutinga hatua ya makundi, ilikubali kipigo cha mabao 2-1 ugenini Zambia kutoka kwa Nkana FC kabla ya kushinda 3-1 katika Uwanja wa Taifa jijini Da es Salaam, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya tofauti ya mabao 5-2.

Kwenye hatua ya makundi, ilianza kwa kushinda nyumbani mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura na kisha ikachapwa 5-0 ugenini DR Congo dhidi ya AS Vita na kipigo tena kama hicho kutoka kwa Al Ahly ikiwa nchini Misri.

Hata hivyo, Simba iliendeleza moto wake ikiwa nyumbani kwa kuichapa Al Ahly bao 1-0 na kisha kwenda ugenini Algeria ambapo ilikubali kulala kwa mabao 2-0 dhidi ya JS Saoura kabla ya kurudi Uwanja wa Taifa kumalizia hasira zake kwa kuifumua AS Vita mabao 2-1.

Habari Kubwa