Chikwende katikati ya Morrison, Kahata

18Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Chikwende katikati ya Morrison, Kahata
  • ***Aapa kupigania namba huku akiwataja Miquissone, Bwalya na Kapombe, lakini...

WAKATI akifurahia kuwa miongoni mwa nyota watakaounda kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara na kuahidi kupambana na ushindani uliopo, winga mpya wa Simba, Mzimbabwe Perfect Chikwende, ameendelea kuwa katikati ya nyota wawili wa timu hiyo, Bernard Morrison na Francis Kahata.

Simba inatarajiwa kutangaza kukata mchezaji mmoja kati ya 10 wa kimataifa ili kumwezesha Chikwende kucheza Ligi Kuu na kama itashindwa kufanya hivyo, nyota huyo aliyejiunga na 'Wekundu wa Msimbazi' hao akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, ataichezea kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa pekee.

Nyota wa kimataifa wa Simba ambao wapo kwenye usajili wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa ni Pascal Wawa (Ivory Coast), Joash  Onyango na Francis Kahata (Kenya), Bernard Morrison (Ghana), Rally Bwalya na Clatous Chama (Zambia), Chris Mugalu (DR Congo), Meddie Kagere (Rwanda), Luis Miquissone (Msumbiji) na Taddeo Lwanga (Uganda).

Simba inatakiwa kuengua mchezaji mmoja kwenye orodha ya watakaocheza Ligi Kuu kutokana na kanuni ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), kuruhusu kila klabu kuwa na wachezaji 10 tu wa kigeni waliosajiliwa kushiriki ligi hiyo.

Hata hivyo, licha ya uongozi wa Simba kutoweka wazi hadi sasa kuhusu mchezaji itakayemuengua ili kumpisha Chikwende kuitumikia klabu hiyo kwenye Ligi Kuu Bara, Morrison na Kahata, wamekuwa wakihusishwa zaidi mmoja kumpisha winga huyo wa Zimbabwe.

Taarifa kutoka chanzo chetu ndani ya klabu hiyo, zimeeleza: "Anaweza kuwa Morrison ama Kahata, lakini bado uamuzi rasmi haujafikiwa, tunataka kufanya hivyo ili kumwezesha Chikwende kuzoeana vizuri na wenzake uwanjani."

Lakini kwa upande wa Chikwende akizungumzia usajili wake, alisema ni mwenye furaha kujiunga na Simba na ni moja ya timu nzuri yenye ushindani mkubwa, hivyo atajitahidi kupambana ili kupata nafasi.

"Kwa ujumla ni mwenye furaha, timu ni nzuri, kuna ushindani mkubwa ambao utaboresha wasifu wangu, nitapambana ili kupata kiwango changu bora," alisema mchezaji huyo ambaye aliifunga Simba wakati FC Platinum ikishinda bao 1-0 nyumbani kwenye mechi ya kwanza ya raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya Wekundu wa Msimbazi hao kupindua matokeo Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa kushinda 4-0 mechi ya marudiano.

Kuhusu majina ya wachezaji anaowafahamu ndani ya timu yake hiyo mpya, Chikwende aliwataja Luis Miquissone, Clatous Chama, Rally Bwalya na Shomari Kapombe, ikionyesha bado ana kumbukumbu ya namna nyota hao walivyowasumbua wakati walipokutana kwenye mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam Januari 6, mwaka huu.

"Luis, Chama, Bwalya na Kapombe ni baadhi ya wachezaji ninaowafahamu katika klabu ya Simba," alisema Chikwende hadi sasa ana mabao mawili kwa jina lake kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Katika mechi hiyo ya marudiano, mabao yalifungwa na Erasto Nyoni (penalti), Kapombe, John Bocco na Chama (penalti) huku Miquissone na Bwalya wakionyesha kiwango cha juu...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa