Chirwa, Msuva kupeleka maumivu Zanaco leo

11Mar 2017
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Chirwa, Msuva kupeleka maumivu Zanaco leo
  • ***Nyota hao wamekuwa kwenye kiwango kikubwa msimu huu, Azam kushuka Uwanjani kesho...

KOCHA wa Yanga, George Lwandamina, amesema hakuna kitakacho wazuia leo kupata ushindi kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika huku akiamini washambuliaji wake, Simon Msuva na Obbrey Chirwa watapeleka kilio kwa wapinzani wao Zanaco.

Yanga inacheza na Zanaco leo kwenye Uwanja wa Taifa kuanzia saa 10:00 jioni ukiwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msuva na Chirwa wamekuwa kwenye kiwango cha juu huku wakiisaidia Yanga kupata ushindi kwenye michezo yao.

Wiki iliyopita Chirwa alionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Kiluvya United na kufunga magoli manne katika ushindi wa bao 6-1 waliupata Yanga.

Msuva, anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji kwenye ligi kuu msimu huu akiwa na magoli 12, amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Yanga na leo anatagemewa kupeleka kilio kwa Wazambia hao.

Akizungumza na gazeti hili jana, Lwandamina, alisema kuwa hana hofu na mchezo wa leo kwa kuwa kila kitu amekiweka sawa na kazi imebaki kwa wachezaji wake tu.

"Naamini kwa kile tulichokifanya mazoezini na kama wachezaji watafuata maelekezo yangu, nina uhakika wa ushindi mzuri kesho (leo)," alisema Lwandamina.

Alisema kuwa anawafahamu wapinzani wao wa leo kwa kuwa amekutana nao mara kwa mara kwenye Ligi ya Zambia wakati alipokuwa akiifundisha Zesco ya nchini humo.

Lwandamina, alisema watacheza soka la kushambulia muda wote na kujaribu kuwabana wapinzani wao wasitengeneze nafasi ya kupata bao litakalovuruga mipango yao.

Mchezo wa leo utachezeshwa na mwamuzi Aden Abdi kutoka Djibout akisaidiwa na Hassan Yacin na Farhan Salime.

Wakati Yanga wakicheza leo Uwanja wa Taifa, wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam FC watashuka Uwanja kesho kuumana na Mbabane Swallows kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Mchezo huo wa hatua ya kwanza umepangwa kuanza saa 1:15 usiku.

Habari Kubwa