Coastal Union yaanza mipango

31Jul 2020
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Coastal Union yaanza mipango

UONGOZI wa Coastal Union umesema hauna wasiwasi wowote kutokana na tetesi za nyota wake waliokisaidia kikosi hicho kufanya vema msimu huu, kutakiwa na klabu nyingine zikiwamo vigogo, Simba na Yanga.

Mwenyekiti wa Coastal Union, Steven Mguto, aliliambia gazeti hili hawana presha kwa sababu wana benchi la ufundi imara ambalo linaweza kuwatengeneza wachezaji wengine na timu yao ikaendelea kufanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mguto alisema tetesi hizo wamezisikia lakini watawaruhusu wachezaji wao kuondoka baada ya klabu zinazowahitaji kukubali kuwalipa kiasi cha fedha wanazotaka.

Kiongozi huyo alisema hawatamzuia mchezaji yoyote kuondoka kama klabu inayomhitaji itakubali kumpatia maslahi bora kwa ajili ya kuendeleza kipaji cha mchezaji husika pamoja na wao ambao wamemkuza nyota huyo.

“Viongozi tulikutana na kujadili suala hilo baada ya kusikia na kuona tetesi juu ya wachezaji wetu, kwa sasa tunachokisubiri ni ripoti ya kocha wetu (Juma Mgunda), tutaangalia wachezaji ambao wanabaki na wale ambao wanaondoka, iwe kwa sababu ya kutakiwa na timu nyingine, halafu tutaanzia hapo."

Aliongeza wamepanga kuanza maandalizi ya msimu ujao mapema na hivyo wamemtaka Mgunda kuwasilisha ripoti yake mapema ili ifanyiwe kazi kwa ufanisi.

Habari Kubwa