Coastal yaipigia hesabu Gwambina

08Apr 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Coastal yaipigia hesabu Gwambina

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema kikosi chake kipo tayari kupata ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Gwambina FC utakaochezwa keshokutwa jijini Mwanza.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mgunda alisema kikosi chake kinatarajiwa kuanza safari ya kuelekea Mwanza leo na wanaamini wakifika huko mapema na kupata muda wa kufanya mazoezi mepesi na kujiweka tayari kwa mechi hiyo.

Mgunda alisema wachezaji wake wamejiandaa kufanya vizuri katika mchezo huo kwa sababu wanataka kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja kutokana na pointi walizonazo.

"Tunahitahi kupata matokeo mazuri bila kujali tunacheza nyumbani au ugenini, kikubwa kwa sasa tunaomba uzima na afya ili maandlizi yaende vizuri, nguvu, akili na mawazo yote yanahitaji kusaka ushindi katika kila mchezo tutakaocheza," Mgunda alisema.

Aliongeza anafahamu ligi inaelekea hatua ya lala salama hivyo kila klabu inahitaji kupambana kuhakikisha inapata matokeo chanya ili kujiweka katika nafasi nzuri.

Habari Kubwa