Coastal yakana kumtimua Mgunda

04May 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Coastal yakana kumtimua Mgunda

​​​​​​​KLABU ya Coastal Union imekanusha taarifa zilizozagaa kuanzia juzi kwenye mitandao ya kijamii kuwa imemfuta kazi kocha wake mkuu, Juma Mgunda kutokana na matokeo mabovu ya timu hiyo.

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Rashid Mgweno, ameeleza kushangazwa na taarifa hizo na kuongeza wao kama viongozi hawajawaza ama kufikiria jambo hilo kutokana na kocha huyo alivyo ndani ya klabu hiyo.

"Tunazikanusha, hazina ukweli wowote, ni taarifa za uongo. Hatujui zimetokea wapi, lakini tunaendelea kuzifuatilia ili tuchukue hatua kwa sababu zimezua taharuki kwa wanachama na mashabiki wetu, sisi viongozi hata na mwenyewe pia," alisema katibu huyo.

Alisema kuwa Mgunda kwenye klabu ya Coastal si kocha tu kama watu wanavyoona kwa nje, lakini amekuwa zaidi ya kocha, kwani kuna vitu amekuwa akiisaidia klabu hiyo kwenye kuisogeza mbele kupata mafanikio.

"Sisi hatumchukulii kama ni kocha, bali ni kiongozi pia, wakati mwingine anafanya majukumu ambayo si ya kiualimu, bali kama kiongozi ambavyo watu wengi hawaelewi ndiyo maana sisi viongozi hatujawahi hata kuwaza kumfukuza, kwa sababu tunajua na tumfahamu," alisema.

Habari Kubwa