Coastal yashikwa Mwanza

22Jul 2021
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Coastal yashikwa Mwanza

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Muungano Tanzania mwaka 1990, Pamba ya Mwanza, walishindwa kutumia vyema Uwanja wa Nyamagana, walipolazimishwa sare ya mabao 2-2 na wageni Coastal Union katika mechi ya kwanza ya mchujo, kusaka timu itakayocheza Ligi Kuu msimu wa 2021/22.

Abdallah Suleiman 'Sopu' aliifungia Coastal Union bao la kwanza sekunde ya 19 kabla ya James Ambrose kuisawazisha Pamba dakika ya 11 na kufanya timu hizo kwenda mapumziko wakiwa sare ya goli 1-1.

Bao la pili la Pamba lilifungwa na Emmanuel Haule kwa penalti wakati Raizin Hafidhi aliisawazishia Coastal Union dakika tatu kabla ya mechi kumalizika.

Kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Hamadi Hilika alifunga mabao matatu maarufu kama 'hat-trick', Mtibwa Sugar ikiichapa Transit Camp ya Dar es Salaam mabao 4-1, kwenye mechi nyingine ya 'play off'.

Kelvin Sabato alifunga pia bao lingine kwa Mtibwa na Karegea Hazanga aliifungia bao la kufutia machozi, Transit Camp.

Hatima ya Coastal Union na Mtibwa Sugar kama zitabaki Ligi Kuu au kuteremka daraja, zitajulikana keshokutwa baada ya mechi za marudiano.

Habari Kubwa