Coulibaly arejea kujifunga Simba

05Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Coulibaly arejea kujifunga Simba

WAKATI Simba ikiwa imebakiza nafasi mbili tu kabla ya kukamilisha usajili wa wachezaji 10 wa kigeni, beki ambaye mashabiki wengi hawamkubali, Muivory Coast Zana Coulibaly ametua nchini kwa mazungumzo ya mkataba mpya na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, imeelezwa.

Muivory Coast Zana Coulibaly

Kwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu Bara, kila klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi 10 wa kigeni na tayari Simba imefikisha wachezaji nane hadi sasa.

Kuelekea msimu mpya wa 2019/20, tayari Simba imeshanasa saini za wachezaji wapya watano wa kigeni, ambao ni mabeki Wabrazil Gerson Fraga Vieira kutoka ATK ya Ligi Kuu ya India na Tairone Santos da Silva kutoka Klabu ya Atletico Cearense FC, mshambuliaji Wilker Henrique da Silva kutoka Bragantino, zote za Daraja la Nne nchini Brazil na viungo Msudan Sharaf Eldin Shiboub Ali Abdalrahman aliyetokea Al Hilal ya Sudan pamoja na winga Deo Kanda kutoka TP Mazembe ya kwao, DR Congo.

Nyota hao wapya wanaungana na wachezaji watatu wa msimu uliopita ambao wameongezewa mikataba mipya, kiungo Mzambia Clatous Chama, straika Mnyarwanda Meddie Kagere na beki Muivory Coast Pascal Wawa, hivyo kufikisha jumla ya wachezaji wa kigeni nane.

Simba bado inahaha kuinasa saini ya mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi anayeitumikia timu yake ya taifa katika michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019, lakini inaonekana kama uhakika wa kumpata umefifia baada ya kumnasa kiungo Mkenya Francis Kahata.

Hivyo ni wazi sasa endapo itamuongeza mkataba Coulibaly itakuwa imekamilisha usajili wa wachezaji 10 wa kigeni na kupeperusha matarajio ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo ya kumuona Okwi akiendelea kuitumikia Simba

Coulibaly ambaye alisaini mkataba wa miezi sita kwa lengo la kuwa mbadala wa Shomari Kapombe aliyeumia, imeelezwa kuwa uwezo wake umemkuna Kocha Mkuu, Patrick Aussems na amependekeza asiachwe msimu ujao.

“Ni kweli Coulibaly kwa sasa yupo hapa jijini tayari kwa mazungumzo na yamefikia mahali pazuri, hivyo muda wowote kuanzia sasa atatangazwa kuwa mali ya Simba kwa mkataba wa miaka miwili,” chanzo chetu cha uhakika ndani ya Simba kilieleza.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Coulibaly pia aliandika amerejea Tanzania.