De Gea: Man Utd ijipange kwa Barca

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
De Gea: Man Utd ijipange kwa Barca

GOLIKIPA wa Manchester United, David de Gea, amewaonya 'Mashetani Wekundu' hao kutakiwa kuimarika kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona.

United leo Jumanne itashuka dimbani ugenini kuivaa Barcelona, wakati ikiwa imefungwa bao 1-0 katika mchezo wa robo fanali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na juzi katika mchezo wa Ligi Kuu England, Man United iliibuka na ushindi dhidi ya West Ham na hivyo De Gea anaona kwamba wana nafasi nzuri ya kuimarisha kikosi chao.

Man United inayonolewa na kocha, Ole Gunnar Solskjaer ilipoteza mechi zake nne kati ya tano zilizopita kabla ya mchezo huo wa Jumamosi ambapo walishinda kwa bao la penalti ya dakika za majeruhi kupitia kwa Paul Pogba na kuweza kupata ushindi 2-1 dhidi ya West Ham katika Uwanja wa Trafford.

Na De Gea amesema kwamba wanatakiwa kuwa kwenye ari nzuri zaidi wakati wakishuka kwenye dimba la Camp Nou ili kuweza kupindua matokeo na kuibuka na ushindi.

"Bila shaka ni mchezo mgumu, lakini kama unataka kuipiga timu kubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, unatakiwa kuwa na wachezaji waliopo kwenye kiwango cha juu," alisema De Gea.

"Unatakiwa kujituma zaidi kwenye mchezo mgumu. Nafikiri tulicheza dhidi ya West Ham, tunatakiwa kuimarika zaidi kwenye mchezo. "Tutatakiwa kucheza na kuhakikisha tunashinda na kupata pointi tatu ili tuweze kufuzu kwa hatua ya nusu fainali.”

Habari Kubwa