Dewji kuisuka upya Simba

09Feb 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Dewji kuisuka upya Simba
  • ***Asisitiza uwezo wa kuwafunga Al Ahly Jumanne upo na ilishawahi...

WAKATI akisema kuwa Simba ina uwezo wa kuwafunga Al Ahly katika mechi ya Kundi D itakayochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Mohammed Dewji amesema kuwa anatarajia kutangaza mchakato mpya wa kuajiri watendaji mbalimbali katika kikosi hicho.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Dewji alisema kuwa tayari wameshazungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi kuelekea mchezo huo wa raundi ya nne wa hatua ya makundi, na kuamini kwamba nafasi ya kufanya vema wanayo.

Dewji alisema kuwa hawajataka tamaa kutokana na kufanya vibaya katika mechi mbili zilizopita huku akiongeza kuwa wanakubali kikosi chao cha Simba hakikuwa imara kupambana na wapinzani wao katika hatua hiyo ya makundi.

Alisema kuwa kikosi chao kimepita katika wakati mgumu katika mechi mbili zilizopita, lakini akaongeza kwamba bodi ya klabu hiyo imejipanga kukisuka upya kikosi chao kwa kuajiri na kusajili wachezaji watakaoendana na mipango ya muda mrefu ya kuchukua ubingwa wa Afrika.

"Mwaka huu ni mpango wetu wa kutetea ubingwa ili tuweze kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, mwaka huu, shabaha yetu mwanzoni ilikuwa ni kufika hatua ya makundi, tunaongelea timu 16...lakini tumefika hapa, tumekuja kushindana, lakini kwenye mpira kuna bahati mbaya, wote mnafahamu tumepata bahati mbaya, mambo yanatokea hayapo kwenye mipango, Kapombe (Shomary) aliumia, Nyoni (Erasto) kiukweli imetutingisha," alisema Dewji.

Aliongeza kuwa malengo yao ya muda mrefu ni kuwa bingwa wa Afrika, hivyo wanahitaji kujipanga zaidi na hiyo ni shabaha yao ya pili ya kutwaa ubingwa wa Afrika.

"Bado tuna nafasi, tumeshawahi kuzifunga timu nyingi za Waarabu hapa Dar es Salaam, bado tuna nafasi,...mchezaji wa 12 ni shabiki, ninawaomba sana WanaSimba, ninaimani tunaweza kuwafunga na tukiwafunga tuna nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika," alimaliza mwekezaji huyo mwenye hisa asilimia 49.

Naye Mwenyekiti wa Simba, Swedi Mkwabi, alisema kuwa wanahitaji zaidi hamasa kutoka kwa Watanzania na nafasi ya kufanya vema katika mchezo huo wanayo.

Mkwabi alisema kuwa uongozi umejipanga kuwaondolea machungu yaliyotokana na kufanya vibaya kwenye mechi mbili zilizopita na ili kuongeza hamasa hiyo, kiingilio cha chini katika mechi hiyo kitakuwa ni Sh. 2,000.