Didier atamaliza watukutu nidhamu Simba - Hitimana

26Jan 2021
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Didier atamaliza watukutu nidhamu Simba - Hitimana

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Thiery Hitimana, amesema anamfahamu vizuri Kocha Mkuu mpya wa Simba, Mfaransa Didier Gomes Da Raso, huku akimwelezea kuwa ni mtu ambaye hana uvumilivu kwa mchezaji anayeonyesha utovu wa nidhamu.

Simba juzi ilimtangaza Didier kuwa kocha mkuu akirithi mikoba ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck aliyeachia ngazi baada ya kuipeleka timu hiyo hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Hitimana alisema Didier aliwahi kuwa bosi wake kipindi akiifundisha Rayon Sports ya Rwanda, hivyo anamfahamu vizuri utendaji wake wa kazi huku akimwelezea kuwa ni mwalimu mwenye misimamo mikali hasa lipokuja suala la nidhamu.

Alisema kocha huyo anapenda kufanya kazi kwa uweledi mkubwa na hawezi kumvumilia mchezaji yeyote kwa suala la utovu wa nidhamu (haangali jina wala umuhimu wake ndani ya kikosi) kwa kuwa yupo ambaye ataonyesha nidhamu mbovu akiamini ni adui namba moja anayekwamisha mafanikio ya klabu.

Hivi karibuni, Simba ilimsimamisha mchezaji wake tegemeo Jonas Mkude kutokana na kile kilichodaiwa ni utovu wa nidhamu na kukosa mechi mbalimbali za ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mechi dhidi ya FC Platinum kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Simba wamepata mtu sahihi wa kufikia malengo yao kwani nimefanya kazi na Didier, namfahamu ni kocha anayewajua vizuri wachezaji wa Afrika, hana uoga kwa mchezaji ambaye atakuwa anaenda kinyume cha mipango yake katika kufanikisha wanafikia malengo yanayotarajiwa.

“Falsafa yake ya kufundisha soka inaendana na Simba, anapenda sana kucheza na mfumo anaotumia, inategemea na wachezaji ambao atawakuta ndani ya timu hiyo, Simba watarajie mazuri kutoka kwa kocha huyo, viongozi na mashabiki wanatakiwa kumsapoti katika majukumu yake," alisema Hitimana.

Alisema kulingana na uwezo wa kocha huyo na kuwa na mbinu nyingi na jinsi ubora wa kikosi cha timu hiyo kilivyo bora, wachezaji wakiwa makini kufuata kile wanachofundishwa ana imani Simba itafanikiwa katika malengo yao ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hitimana alisema maslahi na ofa ambazo zinakwenda mezani kwa Didier ni sababu kubwa ambayo inamfanya aondoke na kuvunja mkataba mapema kabla ya muda wake kumalizika katika klabu mbalimbali alizozifundisha.

Habari Kubwa