Dirisha la usajili lafungwa Z'bar

16Oct 2020
Hawa Abdallah
Zanzibar
Nipashe
Dirisha la usajili lafungwa Z'bar

KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), jana lilikamilisha mchakato wa usajili na uhamisho wa wachezaji kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar na Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja, imeelezwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa ZFF, Ali Mohmmed Ameir, alisema mchakato huo umekuwa mwepesi kwa msimu huu, ikilinganishwa na msimu uliopita kwa sababu ya kuuendesha kwa mfumo tofauti.

Ameir alisema msimu huu timu zilijaza fomu zao kwa njia ya kompyuta wakati mwaka jana walitumia mfumo wa karatasi ambayo huitwa 'fomu mama'.

Alisema mchakato huo wa kupitia fomu za usajili ulihusisha timu 12 zitakazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar na nyingine 12 zitakazochuana kwenye Ligi Daraja la Kwanza Kanda ya Unguja pamoja na baadhi ya timu, ambazo zipo katika ngazi za mikoa.

Alitaja changamoto kubwa iliyojitokeza katika usajili huo ni kubainika kwa baadhi ya wachezaji kuwa na mikataba na timu zao za awali, lakini kuomba kuhamishwa kwenda katika klabu mpya.

Kiongozi huyo alivitaka vilabu vyote kuwasilisha nakala za mikataba ya wachezaji wao, ili kuepuka matukio ya kusajiliwa na timu zaidi ya moja.

"Tunazipongeza klabu kwa kufanya mchakato wa usajili kuwa mwepesi, lakini tunawakumbusha kuwasilisha nakala za mikataba, hii itasaidia kubaini wachezaji ambao, wamezungumza na timu zaidi ya moja," aliongeza Ameir.

Wakati huo huo, ZFF kwa kushirikiana na Kamati ya Waamuzi Zanzibar, imefungua mafunzo ya waamuzi wanawake katika Mkoa wa Kusini Unguja na yatakuwa ya miezi mitatu.

Habari Kubwa