Djuma awapeleka Simba robo fainali

15Mar 2019
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe
Djuma awapeleka Simba robo fainali

ALIYEKUWA Kocha Msaidizi wa Simba Mrundi, Masoud Djuma ameipa nafasi timu hiyo kusonga mbele katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwafunga AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini amewataka wawe makini na watulivu zaidi.

Simba itakuwa mwenyeji wa AS Vita katika mechi ya mwisho ya Kundi D itakayochezwa kesho kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Djuma alisema kuwa ili Simba wapate ushindi na watinge hatua ya robo fainali ya mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wanatakiwa kuwadhibiti vema viungo na washambuliaji wa AS Vita.

Djuma alisema kuwa hakuna timu isiyofungika na Simba wanatakiwa kusahau matokeo waliyopata katika mchezo wa kwanza wakati walipokutana na Wakongomani hao.

Kocha huyo wa AS Kigali inayishiriki Ligi Kuu Rwanda alisema kuwa faida ya kucheza nyumbani pia itawaongezea Simba nguvu ya kufanya vizuri katika mchezo huo utakaochezeshwa na waamuzi kutoka Morocco.

"Ni mechi ngumu lakini ninaipa Simba nafasi ya kushinda bao 1-0, kikubwa wawe makini kuwazuia AS Vita mbele na kati, hizo sehemu mbili wako vizuri," alisema mchezaji huyo wa zamani wa APR ya Rwanda.

MAKAMBA KUONGOZA

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara alisema kuwa wachezaji wao wanafahamu umuhimu wa mchezo huo ambao kauli mbiu yake ni "Do or Die" na kujipanga kuwapa furaha mashabiki wao.

"Ni mchezo mgumu kama tulivyocheza mechi nyingine, lakini huu ni Do or Die, hatuna kitu kingine tunachoweza kusema, njooni kwa Mkapa kushuhudia," alisema.

Alimtaja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba ndiye atakuwa mgeni rasmi katika mchezo huo ambao pia utashuhudiwa na shabiki wao mtoto, Rackeem kutoka jijini Tanga.

Simba yenye pointi sita ndio inaburuza mkia katika kundi hilo linaloongozwa na JS Saoura yenye pointi nane ikifuatiwa na Al Ahly yenye pointi saba sawa na AS Vita.

Habari Kubwa