Domayo: Sikudhamiria kumuumiza Kapombe

03Jul 2020
Faustine Feliciane
Dar es Salaam
Nipashe
Domayo: Sikudhamiria kumuumiza Kapombe

KIUNGO wa mabingwa watetezi wa Kombe la FA, Azam FC, Frank Domayo, amwomba msamaha beki wa pembeni wa Simba, Shomari Kapombe na kuongeza hakudhamiria kumuumiza nyota huyo.

KIUNGO wa mabingwa watetezi wa Kombe la FA, Azam FC, Frank Domayo:PICHA NA MTANDAO

Domayo alimkanyaga Kapombe sekunde chache kabla ya mechi ya hatua ya robo fainali ya Kombe la FA kati ya Simba na Azam kumalizika, rafu iliyopelekea beki huyo kuondolewa uwanjani kwa machela.

Kitendo hicho cha Domayo cha kumkanyaga Kapombe wakati wakiwania mpira uliokuwa ukimilikiwa na Kapombe kiliamsha hasira kwa beki huyo aliyeonekana kuchukizwa pamoja na wachezaji wengine wa timu hiyo pamoja na kocha wa viungo, Adel Zrane.

Akizungumza gazeti hili jana, Domayo, alisema hakufanya kitendo hicho kwa makusudi kama ambavyo baadhi ya mashabiki walivyotafsiri isipokuwa tukio hilo lilitokea katika hali ya kawaida ya kuwania mpira.

"Namwomba radhi rafiki yangu Kapombe, sikuwa na dhamira ya kumuumiza, najua ameumia, lakini naomba nieleweke ni kitendo cha bahati mbaya," alisema Domayo.

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga alisema ilikuwa ni 'presha' ya mchezo na tukio hilo lilikuwa la kugombania mpira ambao walikuwa wanaukimbiza wote.

"Nimeumia sana baada ya kuona Kapombe ameumia na namna tukio lenyewe lilivyochukuliwa na mashabiki pamoja na wadau wa mpira, sikufanya kwa makusudi," aliongeza Domayo.

Katika mchezo huo, Simba iliwavua ubingwa wa michuano hiyo, Azam baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 na kusonga mbele katika michuano hiyo inayotarajiwa kuendelea tena kati ya Julai 11 na 12, mwaka huu.

Habari Kubwa